Published December 22, 2019 by with 0 comment

Ubunifu wa Jengo (Building Design) – Hatua Muhimu za Kuzingatia




Habari ya leo rafiki yangu na mfatiliaji wa makala hizi bora za ujenzi! Natumaini unaendelea kupambana kwa hali na mali ili kuhakikisha unakuwa na sehemu bora kabisa ya kuishi unapokuwa hapa duniani. Lengo langu ni kuhakikisha kila mtanzania anapata maarifa sahihi na ya kutosha kuhusu ujenzi wa nyumba ili aweze kuchukua hatua sahihi.

Ubunifu Wa Jengo
Ubunifu wa jengo ni hatua ya awali kabisa kwenye ujenzi wa nyumba yako. Hii ni hatua inayokupa picha halisi ya aina ya nyumba utakayojenga kabla hata hujaanza kufanya ujenzi wa nyumba yako. Pamoja na umuhimu mkubwa wa hatua hii watu wengi wamekuwa wakiikwepa aidha kwa kujua au kutokujua hali inayosababisha kujengwa kwa nyumba za ajabu ajabu huko mtaani.

Nani Wanahusika Kwenye Ubunifu wa Jengo
Kutegemeana na aina/ukubwa wa nyumba unayojenga, mara nyingi utahitaji wataalamu wafuatao; Mtaalamu wa kwanza ni Msanifu Majengo (Architect), Mtaalamu wa pili ni Mhandisi Majengo (Structural Engineer) na mtaalamu wa tatu ni Mkadiriaji Majenzi (Quantity Surveryor). Watu hawa ukiwatumia vizuri una uhakika wa kupata jengo zuri, imara, salama na la gharama nafuu utakalolipenda maisha yako yote. Kujua zaidi kuhusu wataalamu hawa SOMA HAPA.


Hatua  Muhimu za Kuzingatia Wakati wa Ubunifu wa Jengo Lako
Rafiki yangu sasa tuangalie ni hatua gani muhimu zinafanyika ili kukamilisha ubunifu wa jengo lako;  
  • Kutembelea Eneo la Ujenzi. 
Hii ni hatua muhimu sana na ndio inayosaidia katika kutengeneza picha ya jinsi muonekano wa jengo lako utakavyokuwa ukilinganisha na kiwanja chako. Shughuli zinazofanyika hapa ni kama vile;
·         Kuangalia jinsi eneo lilivyo (kama kuna mwinuko, bonde, jiwe kubwa au changamoto yoyote nyingine)
·         Kuchunguza aina ya udongo uliopo eneo la kazi (kama ni eneo la kichanga, au mfinyanzi, au tope, au mawe n.k)
·         Kuoanisha matumizi ya jengo na kiwanja
·         Kuamua mwelekeo wa upande wa mbele wa jengo
·         Kuchukua vipimo halisi vya kiwanja

  •  Kujua Hitaji la Mteja
Hapa unakaa na mtaalamu wa ujenzi na kisha mnakubaliana aina ya nyumba unayoitaka na hapa kuna mambo mengi ya kugusia ikiwemo; muonekano wa nje wa jengo, idadi ya vyumba, aina za vyoo, kimo cha nyumba kwa kwenda juu, aina ya paa, aina ya rangi pamoja na mambo mengine mengi! Mtaalamu wa ujenzi atakushauri vizuri ni kitu gani kinafaa zaidi kwenye nyumba yako kulingana na aina ya maisha unayoishi. Hapa ndipo wazo kuu la nyumba hupatikana tayari kwa kuanza kufanyiwa kazi na mtaalamu wa ujenzi.

  • Kufanya Ubunifu wa Jengo
Kwenye hatua hii sasa wataalamu wa ujenzi wanatumia elimu yao ya sayansi ya mahesabu kupangilia muundo wa nyumba yako na kuipa muonekano mzuri kabisa kulingana na eneo lako lilivyo. Kama utaweza kuwatumia wataalamu wote watatu ni vizuri zaidi lakini endapo unaona uwezo wako ni mdogo basi hakikisha unatumia hata mtaalamu mmoja tu atakayekushauri na kukusaidia katika ubunifu. Jambo la kufurahisha ni kwamba kwa sasa wataalamu hawa wapo wengi na gharama za ubunifu ni ndogo sana ukilinganisha na ujenzi unaoenda kuufanya. Katika hatua hii utategemea kupata yafuatayo;
·         Kupata michoro kutoka kwa msanifu majengo (Architect)
·         Kupata michoro/Ushauri kutoka kwa mhandisi majengo (Structural Engineer)
·         Kupata makadirio ya jumla ya ujenzi wa nyumba yako
  •       Kuomba kibali cha ujenzi Manispaa
Hii ni hatua ya mwisho katika kukamilisha taratibu za ubunifu kabla ya kuanza ujenzi wa jengo lako. Baada ya michoro yote kukamilika na wewe mwenye eneo kuridhika na ubunifu uliofanyika, hatua inayofata ni kuomba kibali cha ujenzi ili kukidhi matakwa ya kisheria. Unapopata kibali cha ujenzi ni kidhibitisho tosha kwamba matumizi ya eneo lako ni sahihi na aina ya ujenzi unaofanya pia ni sahihi. Katika hatua hii mambo mawili muhimu ynafanyika;
·         Kupiga muhuri  na kuweka sahihi kwenye michoro yote (michoro ya msanifu majengo na michoro ya mhandisi majengo)
·         Kupeleka michoro hiyo pamoja na mahesabu ya ubunifu Manispaa kwa ajili ya mchakato wa kupata kibali.

Mpaka hapo rafiki yangu unakuwa umekamilisha hatuma muhimu sana ya ubunifu wa jengo lako. Kinachofata ni watu wa manispaa kuja kukutembelea ili kujiridhisha matumizi ya kiwanja chako na kuona kama michoro iliyoandaliwa inakidhi matakwa ya kisheria.

Hatua  Za Kuchukua
Ili kuwa na nyumba bora ni lazima ufanye uwekezaji bora. Kwanza kabisa jua kwa hakika nini unahitaji linapokuja swala la nyumba, Pili anza kuwekeza kidogo kidogo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yako, Tatu mtafute mtaalamu wa ujenzi na kisha fata hatua nilizoelekeza hapo juu! 

Rafiki yangu hakikisha haufanyi ujenzi kiholela! Gharama za ubunifu ni ndogo, ndogo, ndogo mnooooo ukilinganisha na gharama za ujenzi wa nyumba yako hivyo huna sababu ya kutofanya ubunifu.

Ni mimi rafiki yako na mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;
Eng Beatus B. Laswai
Blog: http://nyumbayakomaishayako.blogspot.com
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
Read More
      edit
Published December 13, 2019 by with 0 comment

Nyumba Bora - Maisha Bora: Mambo Muhimu Unayohitaji Kuyafahamu Ili Uweze Kumiliki Nyumba Bora Ya Kuishi







Nyumba Bora ni Ipi?
Rafiki yangu mpendwa, moja ya hitaji muhimu sana kwa binadamu yeyote yule ni kuwa na Makazi (Nyumba bora) kwa ajili yake pamoja na familia yake. Pamoja na umuhimu huu mkubwa wa nyumba, bado watu wengi hawajatilia mkazo katika kuhakikisha wanapata nyumba bora na mazingira bora ya kuishi. Katika maeneo mengi ya nchi yetu ujenzi wa kiholela usiofata taratibu umekuwa ni jambo la kawaida kitu ambacho kinasababisha watu kuishi kwenye miundo mbinu mibovu kabisa.

Siku ya leo hebu tutafakari….. Ukisikia neno “Nyumba Bora” kichwani mwako unapata picha gani? Je ni kitu gani kila mtu anayefikiria kufanya ujenzi anatakiwa afanye ili aweze kuwa na nyumba bora?

Hebu tuanze na hili la *Nyumba Bora*;
Kwa kifupi, Nyumba bora ni ile ambayo inakidhi mahitaji ya mteja (mwenye nyumba), Iliyojengwa kwa kufuata taratibu na sheria za majenzi na ambayo ipo kwenye mazingira safi, tulivu na salama. Zifuatazo ni sifa ambazo kwa pamoja zinasaidia katika kuwa na nyumba bora;

  • Kufanya ujenzi katika eneo linalokubalika kisheria.
Kuna baadhi ya maeneo huwa yanatengwa kwa ajili ya shughuli maalumu kama vile maeneo ya wazi, maeneo ya viwanda n,k. Hata ujenge nyumba nzuri kiasi gani kama imejengwa eneo ambalo halikubaliki kisheria unakuwa umepoteza thamani ya kuwa na nyumba bora maana muda wowote unaweza kuingia kwenye changamoto ya kubomolewa na kuondolewa kwenye eneo hilo.
  •  Kufata ushauri wa wataalamu wa ujenzi.
Nyumba nyingi zinapoteza ubora na thamani wakati wa ujenzi kutokana na kujengwa chini ya kiwango. Nyumba bora ni ile ambayo imezingatia na kufata ushauri wa mtaalamu wa ujenzi kwa kuzingatia mahitaji ya mteja na sehemu nyumba inapojengwa. Hata kama unajenga nyumba ndogo kiasi gani ni vizuri ukahusisha mtaalamu wa ujenzi angalau kukupa ushauri na kukupa mwanga ufanye nini.
  •  Upatikanaji wa mahitaji muhimu ya binadamu.
Nyumba yako ili iwe bora lazima iwe inafikika kiurahisi, iwe karibu na huduma za kijamii, iwe na uwezekano wa kupata huduma za maji, umeme na mahitaji mengine muhimu ikiwemo huduma za kiusalama.
  •  Matunzo / Usafi wa nje na ndani
Hili ni eneo ambalo watu wengi hasa maeneo ya mijini hawalitilikii mkazo sana. unakuta watu wamezungukwa na uchafu, rangi ya nyumba inabanduka, mabomba yanavuja na mambo mengine madogo madogo lakini hawajali. Unapoishi mazingira yenye uchafu unajiweka katika hatari ya magonjwa, rangi ya nyumba kubanduka kunasababisha kupoteza mvuto wa nyumba, maji maji kutokana na mabomba kuvuja inaweza kuleta shida kwenye mhimili wa jengo. Ili nyumba yako iwe bora ni lazima uijali na kuitunza ili isikuingize kwenye gharama zinazoweza kuzuilika.



*Je ufanye nn ili uweze kuwa na nyumba bora? *

Baada ya kujua sifa za nyumba bora, kinachofata ni kuchukua hatua sahihi ili uweze kumiliki kitu kilicho bora kabisa. Ukifuata ushauri ufuatao utakuwa umejiwekea misingi imara ya kuhakikisha unakuwa na nyumba bora ya kuishi ambayo utaipenda na kuifurahia kila wakati;
  • Kwa wale ambao hawajaanza ujenzi wa nyumba; jambo la kwanza weka malengo sahihi kuhusu aina ya nyumba unayoitaka na lini hasa unaitaka. Lazima ujue kwa hakika ni aina gani ya nyumba unahitaji (Hapa unaweze kushauriana na mtaalamu wako wa ujenzi na ukapata wazo bora kabisa). Watu wengi wanashindwa kuwa na nyumba bora kwa sababu hawaweki lengo maalumu na mwisho wa siku wanajikuta wanafanya ujenzi ghafla ghafla tena kwa mazoea.
  • Jambo la pili ni kuchukua hatua na hatua muhimu hapa ni kuanza kuwekeza kwa ajili ya nyumba yako. Anza na kiwango kidogo kabisa huku ukijipa hamasa kila siku. Usikurupuke tu na kuanza kujenga nyumba kwa kutumia fedha za mshahara au biashara. Nyumba ya kuishi kama tulivyoona kwenye kitabu cha “”Rich Dad Poor Dad”” ni Liability (inakuondolea pesa mfukoni) hivyo ni muhimu uwe na account maalumu ili usije ukaingia kwenye madeni au kusababisha kuyumba kwa biashara. 
  • Tafuta mtaalamu wa ujenzi kwa ajili ya kupata ushauri na kutengeneza picha ya jengo lako. Siku hizi kuna mbinu nyingi na mpya za ujenzi ambazo zinaweza kukusaidia katika kupata nyumba bora kwa gharama nafuu kabisa. Mtaalamu wa ujenzi akishajua mahitaji yako ni rahisi kukushauri njia sahihi ya kuchukua ili ufikie lengo lako. Hapa utapata elimu sahihi kuhusu matumizi ya kiwanja chako, sharia za majenzi, nini ufanye kabla ya ujenzi, wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi.
  • Anza Sasa. Ukitaka uzuri sharti uzurike; ukitaka nyumba bora inabidi ujitoe kwelikweli na usisubiri mpaka mambo yakae vizuri ndo uanze, ANZA SASA. Kinachowafanya watu wengi kujenga nyumba zisizo na ubora ni kufanya ujenzi kwa pressure bila kuwa na mpangilio maalumu.

Kuwa na nyumba bora utakayoifurahia muda wote ni jambo linalowezekana kabisa.

Kwa ushauri, maoni au maswali usisite kuwasiliana nami……
Jina: Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com

Read More
      edit
Published December 06, 2019 by with 0 comment

Tofauti Kati ya Kiwanja Kilichopimwa (Surveyed Plot) na Kiwanja ambacho hakijapimwa (Unsurveyed Plot)





Kuwa na taarifa sahihi za ujenzi kabla na wakati wa ujenzi ni jambo la muhimu sana katika zama hizi kwa yeyote yule anayefikiria kujishughulisha na shughuli za ujenzi. Tumekuwa tukiona watu mbalimbali wakiingia kwenye matatizo ya kubomolewa nyumba zao na wengine wakipoteza ardhi wanazomiliki au kuingia kwenye migogoro isiyoisha kutokana na kukosa taarifa na maarifa sahihi kabla ya kufanya ujenzi.

Rafiki yangu mpendwa, kama unafikiria kufanya shughuli yeyote ya ujenzi; Moja ya vitu muhimu kabisa vya kuzingatia kabla hujaanza ujenzi ni kujua kama eneo unalotaka kujenga limepimwa au halijapimwa. Na hapa ndipo tunaenda kujadili kwa kina ambapo tutaangalia mambo matatu muhimu;
  1. Tofauti kati ya Kiwanja kilichopimwa (Surveyed Plot) na ambacho hakijapimwa (Unsurveyed plot)
  2. Faida ya Kufanya ujenzi kwenye kiwanja Kilichopimwa 
  3. Hasara za kufanya ujenzi kwenye kiwanja ambacho hakijapimwa

*Tuanze moja kwa moja na tofauti baina ya kiwanja kilichopimwa na ambacho hakijapimwa.*
Kiwanja kilichopimwa ni kile ambacho kina hati na kinaonyesha mmiliki halali wa eneo hilo iwe ni kwa mauziano, kwa kurithi au hata kwa kupewa zawadi. Eneo hili linakuwa limeonyeshwa kwenye ramani ya mipango miji ambapo inakuwa imeonywesha ukubwa wa eneo kwa vipimo halisi pamoja na matumizi sahihi ya eneo husika kulingana na mahitaji ya mipango miji. Utalitambua eneo hili kwa kuangalia alama za mawe yaliyowekwa kwenye kona za kiwanja.

Kwa upande wa pili, kiwanja kisichopimwa ni kile ambacho hakina hati. Mara nyingi haya ni maeneo ambayo yanakuwa nje ya miji na yanakuwa chini ya usimamizi wa halmashauri za vijiji. Maeneo haya yanakuwa hayana ramani rasmi ya mipango miji na hivyo huwa hakuna mpangilio rasmi wa matumizi ya maeneo haya.

*Pili tuangalie faida za kufanya ujenzi kwenye eneo lililopimwa*
Baada ya kuona tofauti ya kiwanja kilichopimwa na ambacho hakijapimwa, zifuatazo ni faida chache kati ya nyingi utakazozipata kwa kujenga kwenye kiwanja kilichopimwa
  • Matumizi ya eneo yanakuwa yameainishwa waziwazi kwa mfano kama ni eneo la makazi, eneo la viwanda, eneo la kanisa/msikiti au eneo la biashara. kwa namna hii ni rahisi kujenga nyumba inayoendana na matumizi ya eneo
  • Maeneo yaliyopimwa kunakuwa na huduma zote za kijamii kuanzia kwenye barabara, maji, maduka, maeneo ya wazi n.k
  • Kutambulika rasmi na serikali kwa uwepo wako kwenye eneo husika na hivyo kuepuka migogoro na changamoto zisizo za lazima.

*Tatu tuangalie hasara za kufanya ujenzi kwenye eneo ambalo halijapimwa..**
Unapojenga kwenye eneo ambalo halijapimwa unakuwa umejiweka kwenye hatari zifuatazo
  • Kutokuwa na uhakika wa matumizi ya eneo husika hali ambayo inaweza kusababisha ujikute unajenga nyumba ya makazi kwenye eneo la viwanda
  •  Uwezekano wa kupoteza nyumba yako pale ramani ya mipango miji itakapotoka na kuonyesha kwamba sehemu uliyojenga inahitajika itumike kwa matumizi mengine.
  • Usumbufu mkubwa wa kuhamishwa kwenye eneo lako na kupewa sehemu nyingine au kulipwa fidia ya kuondoka kwenye eneo lako

Ndugu msomaji hayo ni mambo machache kati ya mengi ambayo unapaswa kuyajua linapokuja swala la kiwanja kilichopimwa au ambacho hakijapimwa. Kabla hujaanza ujenzi wako ni vyema ukajiridhisha kwa 100% kwamba unajenga sehemu sahihi ambapo hutategemea kupata usumbufu labda itokee majanga ya asili.

*Ushauri wangu kwako*
Kwa wale wenye maeneo ambayo hayajapimwa ni vyema wakachukua hatua stahiki za kwenda manispaa kuomba ramani ya mipango miji ili waweze kujua kuhusu mpangilio wa maeneo yao. Endapo itatokea manispaa hakuna ramani ya mipango miji basi inabidi waombe kupimiwa maeneo hayo kabla hawajaanza kuyaendeleza na hata kama wameshayaendeleza basi waombe ufanyike urasimishaji wa maeneo hayo ili waweze kutambulika rasmi kama wamiliki halali. Kwa kuwa gharama za upimaji zinaweza kuwa juu kama ukiwa peke yako,, basi nashauri pia watu wenye maeneo yaliyo karibu karibu na hayajipwa wajikusanye pamoja na kwenda kuomba upimaji ili kupunguza gharama hizo.

Mbali na hayo niliyokueleza hapo juu kumbuka pia kuwasiliana na mshauri / mtaalamu wako wa ujenzi ili aweze kukushauri na kukusaidia katika kufuatilia baadhi ya vitu muhimu kabla ya kuanza ujenzi wako.

Muhimu zaidi tuhakikishe tunajenga katika maeneo yaliyoainishwa vizuri ili kuepuka usumbufu kwa siku za mbeleni. Pia kwenye kununua ardhi tukumbuke kuna matapeli ambao wanaweza kukuingiza hasara mara mbili. 

Nikutakie kila la kheri katika kuhakikisha unakuwa na nyumba bora ya kuishi iliyojengwa katika sehemu bora kabisa.

Rafiki yako mpendwa katika ujenzi wa taifa bora
Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084
Email:engbeatus.laswai@gmail.com
Read More
      edit