Habari ya leo
rafiki yangu na mfatiliaji wa makala hizi bora za ujenzi! Natumaini
unaendelea kupambana kwa hali na mali ili kuhakikisha unakuwa na sehemu bora
kabisa ya kuishi unapokuwa hapa duniani. Lengo langu ni kuhakikisha kila
mtanzania anapata maarifa sahihi na ya kutosha kuhusu ujenzi wa nyumba ili aweze kuchukua
hatua sahihi.
Ubunifu Wa Jengo
Ubunifu wa jengo
ni hatua ya awali kabisa kwenye ujenzi wa nyumba yako. Hii ni hatua inayokupa
picha halisi ya aina ya nyumba utakayojenga kabla hata hujaanza kufanya ujenzi
wa nyumba yako. Pamoja na umuhimu mkubwa wa hatua hii watu wengi wamekuwa
wakiikwepa aidha kwa kujua au kutokujua hali inayosababisha kujengwa kwa nyumba
za ajabu ajabu huko mtaani.
Nani Wanahusika Kwenye Ubunifu wa Jengo
Kutegemeana na aina/ukubwa wa nyumba unayojenga, mara nyingi utahitaji wataalamu wafuatao;
Mtaalamu wa kwanza ni Msanifu Majengo
(Architect), Mtaalamu wa pili ni Mhandisi Majengo (Structural Engineer) na mtaalamu wa tatu ni Mkadiriaji Majenzi (Quantity Surveryor). Watu hawa ukiwatumia vizuri una
uhakika wa kupata jengo zuri, imara, salama na la gharama nafuu utakalolipenda maisha yako yote. Kujua zaidi kuhusu wataalamu hawa SOMA HAPA.
Rafiki yangu
sasa tuangalie ni hatua gani muhimu zinafanyika ili kukamilisha ubunifu wa
jengo lako;
- Kutembelea Eneo la Ujenzi.
Hii ni hatua muhimu sana na ndio inayosaidia katika kutengeneza picha ya jinsi muonekano wa jengo lako utakavyokuwa ukilinganisha na kiwanja chako. Shughuli zinazofanyika hapa ni kama vile;
·
Kuangalia jinsi eneo lilivyo
(kama kuna mwinuko, bonde, jiwe kubwa au changamoto yoyote nyingine)
·
Kuchunguza aina ya udongo
uliopo eneo la kazi (kama ni eneo la kichanga, au mfinyanzi, au tope, au mawe
n.k)
·
Kuoanisha matumizi ya jengo na
kiwanja
·
Kuamua mwelekeo wa upande wa
mbele wa jengo
·
Kuchukua vipimo halisi vya
kiwanja
- Kujua Hitaji la Mteja
Hapa unakaa na mtaalamu wa ujenzi na kisha mnakubaliana aina ya nyumba unayoitaka na hapa kuna mambo mengi ya kugusia ikiwemo; muonekano wa nje wa jengo, idadi ya vyumba, aina za vyoo, kimo cha nyumba kwa kwenda juu, aina ya paa, aina ya rangi pamoja na mambo mengine mengi! Mtaalamu wa ujenzi atakushauri vizuri ni kitu gani kinafaa zaidi kwenye nyumba yako kulingana na aina ya maisha unayoishi. Hapa ndipo wazo kuu la nyumba hupatikana tayari kwa kuanza kufanyiwa kazi na mtaalamu wa ujenzi.
- Kufanya Ubunifu wa Jengo
Kwenye hatua hii sasa wataalamu wa ujenzi wanatumia elimu yao ya sayansi ya mahesabu kupangilia muundo wa nyumba yako na kuipa muonekano mzuri kabisa kulingana na eneo lako lilivyo. Kama utaweza kuwatumia wataalamu wote watatu ni vizuri zaidi lakini endapo unaona uwezo wako ni mdogo basi hakikisha unatumia hata mtaalamu mmoja tu atakayekushauri na kukusaidia katika ubunifu. Jambo la kufurahisha ni kwamba kwa sasa wataalamu hawa wapo wengi na gharama za ubunifu ni ndogo sana ukilinganisha na ujenzi unaoenda kuufanya. Katika hatua hii utategemea kupata yafuatayo;
·
Kupata michoro kutoka kwa
msanifu majengo (Architect)
·
Kupata michoro/Ushauri kutoka kwa
mhandisi majengo (Structural Engineer)
·
Kupata makadirio ya jumla ya
ujenzi wa nyumba yako
- Kuomba kibali cha ujenzi Manispaa
Hii ni hatua ya mwisho katika kukamilisha taratibu za ubunifu kabla ya kuanza ujenzi wa jengo lako. Baada ya michoro yote kukamilika na wewe mwenye eneo kuridhika na ubunifu uliofanyika, hatua inayofata ni kuomba kibali cha ujenzi ili kukidhi matakwa ya kisheria. Unapopata kibali cha ujenzi ni kidhibitisho tosha kwamba matumizi ya eneo lako ni sahihi na aina ya ujenzi unaofanya pia ni sahihi. Katika hatua hii mambo mawili muhimu ynafanyika;
·
Kupiga muhuri na kuweka sahihi kwenye michoro yote (michoro
ya msanifu majengo na michoro ya mhandisi majengo)
·
Kupeleka michoro hiyo pamoja na
mahesabu ya ubunifu Manispaa kwa ajili ya mchakato wa kupata kibali.
Mpaka hapo
rafiki yangu unakuwa umekamilisha hatuma muhimu sana ya ubunifu wa jengo lako.
Kinachofata ni watu wa manispaa kuja kukutembelea ili kujiridhisha matumizi ya
kiwanja chako na kuona kama michoro iliyoandaliwa inakidhi matakwa ya kisheria.
Hatua Za Kuchukua
Ili kuwa na nyumba bora ni lazima ufanye uwekezaji bora. Kwanza kabisa jua kwa hakika nini unahitaji linapokuja swala la nyumba, Pili anza kuwekeza kidogo kidogo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yako, Tatu mtafute mtaalamu wa ujenzi na kisha fata hatua nilizoelekeza hapo juu!
Rafiki yangu hakikisha haufanyi ujenzi kiholela! Gharama za ubunifu ni ndogo, ndogo, ndogo mnooooo ukilinganisha na gharama za ujenzi wa nyumba yako hivyo huna sababu ya kutofanya ubunifu.
Ni mimi rafiki
yako na mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129
412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
0 comments:
Post a Comment