Published August 04, 2018 by with 2 comments

Fahamu Chanzo cha Nyufa (Cracks) Kwenye Nyumba na Namna Bora ya Kutibu Mipasuko Hii


Rafiki yangu, tatizo la nyufa kwenye nyumba ni moja ya changamoto zinazowasumbua watu wengi sana wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi. Inawezekana kabisa umeshawahi kukutana na changamoto hii au uliona changamoto hii kwa mtu mwingine na hukujua ufanye nini ili uweze kuitatua. Leo rafiki yangu tutakwenda kujifunza kuhusu nyufa kwenye nyumba, chanzo chake na namna bora kabisa ya kudhibiti mipasuko hii.

Nyufa (Cracks) ni Nini?

Nyufa ni mipasuko midogomidogo au mikubwa inayotokea sehemu mbalimbali za nyumba yako kama vile kwenye kuta, slab, nguzo, kona za madirisha na milango na kwenye msingi. Kwa ufupi nyufa ni alama ya uzaifu (tatizo) kwenye sehemu husika ya jengo lako. Udhaifu huu una madhara mengi ikiwemo kuharibu mvuto wa nyumba na Zaidi kupunguza ubora na uimara wa jengo lako. Huwezi kukaa kwa Amani ndani ya nyumba yenye mipasuko.

 

 

Nini Hasa Kinasababisha Nyufa kwenye Jengo?

Kuna sababu nyingi sana ambazo zinachangia katika kusababisha nyufa kwenye nyumba Lakini leo naomba tuangalie sababu kuu sita ambazo ndizo huchangia kwa kiasi kikubwa;
i.                 Ujenzi wa mazoea: Unaweza ukawa unashangaa kwamba hili linawezekana vipi ila hii ni moja ya sababu kubwa sana katika kuzalisha nyumba mbovu na ambazo hazidumu. Kujenga kwa mazoea ni ule ujenzi wa kiholela usiofuata taratibu za majenzi ambapo mtu anafanya ujenzi bila kuhusisha mtaalamu yeyote wa ujenzi. Watu wengi wanafanya hivi eti ili kukwepa gharama wakiamini kwamba kutumia mtaalamu kutaongeza gharama kumbe wanajiingiza kwenye matatizo makubwa Zaidi. Kwenye ujenzi kuna vitu vingi sana vya kuangalia kuanzia kwenye aina ya udongo, uzito wa nyumba, eneo la ujenzi, uwepo wa maji maji, mitikisiko ya ardhi na mengine mengi. Mambo yote haya yanahitaji uwepo wa mtaalamu (engineer au fundi mzoefu) ili aweze kukupa ushauri sahihi kulingana na mazingira ya eneo lako.
Muhimu: Unapofanya ujenzi usiangalie kukwepa gharama tu, fikiria pia kuhusu usalama na ubora wa jengo lako!
ii.                Mchanganyo usio sahihi wa malighafi wakati wa ujenzi. Mfano unapoandaa mortar ya kuunganisha tofali na tofali inakubidi uchanganye vizuri cement, mchanga na maji katika mlinganyo sahihi. Endapo fundi atakosea basi tegemea kupata nyufa
iii.               Kutitia kwa msingi (foundation settlement): Hii inatokea mara nyingi kama nyumba imejengwa kwenye kina kisicho imara
iv.              Nguvu za asili za kimazingira kama vile matetemeko na upepo mkali. Haya mara nyingi tunaweza kuyadhibiti kwa kiwango kidogo sana na wakati mwingine hatuwezi kabisa kudhibiti hali hizi.
v.                Kutumia malighafi mbovu; Watu wengi wanapenda vitu vya rahisi rahisi na hujikuta wakinunua malighafi za bei ndogo ambazo mara nyingi ni dhaifu. Kuwa makini unapochagua malighafi za ujenzi usije ukaikimbia nyumba yako baadae.
vi.              Kutumia mbinu zisizo sahihi za ujenzi: mbinu za ujenzi kwenye eneo lenye majimaji ni tofauti kabisa na ujenzi kwenye eneo kavu lisilo na maji, kuwa makini kabla hujaanza ujenzi, Fundi anaweza akawa mzuri sana kwenye eneo moja lakini akashindwa vibaya kwenye eneo jingine.

                                

                                     

Je Unawezaje Kuondoa Tatizo Nyufa kwenye Nyumba Yako

Unapotaka kutibu tatizo la nyufa kwenye nyumba yako ni vyema kujua chanzo hasa cha nyufa hizo ni nini na ukubwa wa athari zake kwenye nyumba ukoje na pia nyufa hiyo imetokea wapi! Kuna nyufa ambazo ni hatari Zaidi kwenye jengo lako na kuna ambazo ni za kawaida (tofauti hii nitaieleza kwenye Makala nyingine) lakini pamoja na kwamba kuna tofauti nyufa zote hizi zinahitaji kutibiwa. Hapa nitakueleza jinsi ya kutibu nyufa kwenye kuta (mortar na tofali) ambayo ndiyo changamoto inayowakumba watu wengi Zaidi;
Ondoa tatizo la nyufa kwenye kuta zako kwa kufanya yafuatayo;
i.                 Angalia kama nyufa yako inaendelea kuongezeka au imeshaacha kuongezeka. Kama bado nyufa inaongezeka basi kuna tatizo Zaidi hapa inabidi umuite mtaalamu aje akague ili akupe mwongozo nini cha kufanya. Kama nyufa imeacha kuongezeka endelea na hatua ya pili hapa chini.
ii.                Tafuta fundi kisha mwambie atindue umbali wa futi 1 kila upande kufuata mpasuko.
iii.               Nunua expanded wiremesh (nyavu ngumu) kama mpasuko wako ni mkubwa au nunua wiremesh za kawaida (mfano nyavu kama zile za banda la kuku) kama ukuta wako una mipasuko midogo. Nunua pia misumari ya zege ili kupigilia wavu wako kwenye ukuta
iv.               Mwambie fundi achanganye mortar kali (cement na mchanga – mlinganyo wa 1:3 unafaa) na kisha achanganye na kiwango sahihi cha maji na kisha apige plaster sehemu uliyoweka nyavu za chuma (wiremesh).
v.                Fundi akimaliza kutengeneza vizuri subiri kwa masaa 12 kisha mwagia maji kila siku asubui na jioni kwa muda wa siku 7 na hapo utakuwa umemaliza kabisa tatizo la nyufa.




Mpaka hapo rafiki yangu tunakuwa tumejifunza mambo muhimu sana kuhusu changamoto za nyufa na jinsi ya kudhibiti nyufa kwenye jengo.

Hatua Za Kuchukua

Kwa wale ambao hawajajenga au wako mbioni kujenga Muda mzuri wa kudhibiti nyufa ni kabla hujaanza ujenzi wa nyumba yako. Jitahidi kuzingatia kanuni za ujenzi zitakusaidia kuepuka mambo mengi sana. Hakikisha angalau kuna mtu mmoja mwenye uelewa kuhusu mambo ya ujenzi atakayekuwa anakushauri kabla na wakati wa ujenzi wa nyumba yako.
Kwa wale ambao wameshajenga na kukutana na changamoto ya nyufa basi wafate hatua nilizoelekeza hapo juu. Kama nyufa yako haipo kwenye ukuta labda imetokea kwenye sakafu au nguzo au eneo jingine basi unaweza ukanitafuta au ukatafuta mtaalamu atakayekuelekeza mbinu sahihi za kutibu tatizo lako.
Marekebisho yoyote unayoyafanya hakikisha unayafanya kwa umakini wa hali ya juu ili kuepuka kuongeza tatizo au kuanzisha tatizo jingine.

Nikutakie kila la kheri katika kuhakikisha unakuwa na nyumba bora na salama kabisa ya kuishi ili maisha yako yazidi kuwa bora.
#JengaKitaalamu
#TumiaWataalamuWaUjenzi
#EpukaKufanyaMakosaYasiyoYaLazima
#OkoaGharamaZaUjenzi

Kwa mahitaji kuhusu ushauri na namna bora ya kufanya ujenzi wa nyumba yako usisite kuwasiliana nami
Jina : Eng Beatus B. Laswai
Blog: http://nyumbayakomaishayako.blogspot.com
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
      edit

2 comments: