Published April 01, 2019 by with 5 comments

Msingi Imara, Nyumba Imara




Moja ya maamuzi mabovu kabisa ambayo hutakiwi kuyafanya linapokuja swala la ujenzi wa nyumba yako ni kutokujenga msingi imara. Ngoja nikupe mfano rafiki; Mmoja wa marafiki zangu wakati nasimamia ujenzi wa nyumba yake maeneo ya Iringa; majirani zake walikuwa wanamwambia tunatumia gharama kubwa sana kwenye msingi kama vile tunajenga ghorofa mpaka ikafika wakati akawa anahisi kama vile anapoteza pesa ya bure. Miezi kadhaa baada ya nyumba yake kukamilika ndipo alipoona umuhimu wa kile tulichokifanya  kwani ilikuwa kipindi cha mvua na nyumba za majirani zake karibu zote zilionyesha mipasuko (cracks). Walichosahau majirani zake ni kwamba eneo lile lina udongo wa mfinyanzi ingawa ulikuwa kwa kiasi kidogo na hivyo ilitakiwa waweke msingi imara kabisa.

Leo rafiki yangu napenda kukushirikisha umuhimu wa kuwa na msingi imara. Utaweza kufahamu msingi imara ni upi na ni kwa namna gani utahakikisha unakuwa na msingi imara kabisa ili ujihakikishie ujenzi wa nyumba bora.



*Msingi Imara* kwa ufupi ni ule ambao unaweza kuhimili uzito wa jengo pamoja na nguvu kutoka nje kama vile upepo, msukumo wa udongo, mitikisiko pamoja na nguvu nyingine za asili. Msingi huu unaweza ukajengwa kwa kutumia mawe, matofali ya block, Zege au malighafi nyingine ambazo zinakubalika kwenye ujenzi. Unapokuwa na msingi imara unajihakikishia usalama wako, mali zako na wote watakaoishi ndani ya nyumba yako na pia utaweza kujikinga kwa namna Fulani na majanga ya asili kama vile matetemeko na mitikisiko ya ardhi.

SOMA HAPA: Hatua Tatu Muhimu Ujenzi wa Msingi Imara

*Namna ya kuhakikisha unajenga msingi imara*
Ili kuweza kujenga msingi imara na utakaosaidia kuimarisha jengo lako zingatia mambo yafuatayo;
i.                 Fanya utafiti wa eneo lako hasa katika kutambua aina ya udongo
Hapa unaweza ukafanya hata utafiti wa macho tu na kwa kushirikiana na mtaalamu wako wa ujenzi ukaweza kufanya maamuzi ya msingi utakaohitajika. Wakati mwingine udongo wa juu ya ardhi unaweza ukawa tofauti na ule uliopo ndani ya ardhi baada ya kuchimba mita kadhaa na endapo utakutana na hali hii basi msingi wako itabidi ubadilike kulingana na aina ya udongo uliyokutana nayo. Cha kuzingatia hapa ni kuhakikisha msingi wako unakaa juu ya sehemu ngumu na imara ili kuepuka kutitia.

ii.               Tambua kama eneo lako lina maji maji au ni eneo kavu
Msingi unaojengwa sehemu zenye majimaji ni tofauti kabisa na msingi utakaojengwa sehemu kavu. Kwa eneo ambalo lina maji muda mrefu msingi wake utahitaji material (mali ghafi) zinazoweza kuhimili uwepo wa maji kama vile zege. Ukijenga msingi wa matofali ya kawaida kwenye eneo hili unajiweka kwenye hatari kubwa sana

iii.             Jua matumizi sahihi ya Jengo lako
Kwa kutambua matumizi sahihi ya jengo lako kunasaidia sana katika kutambua uzito sahihi utakaohitajika kubebwa na msingi wako. Msingi wa nyumba ya kuishi ni tofauti sana na msingi wa ghala hivyo usijenge nyumba ya kuishi hafu baada ya muda unaibadilisha na kuwa ghala utaleta matatizo kwenye msingi.

Ninachotaka kukukumbusha rafiki yangu leo ni kwamba msingi ndio sehemu ya kwanza muhimu kwenye jengo lako na kamwe hutakiwi kufanya makosa kwenye eneo hili.


Kitu kingine ambacho ningependa kusisitiza ni kwamba USIJENGE KWA MAZOEA. Epuka kabisa maneno ya mtaani eti mbona Fulani amejenga hivi au vile na wewe ukayapokea yalivyo. Itakapotokea tatizo itakuwa ni wewe na wale watakaokuwa wanaishi ndani ya nyumba hiyo.

Jenga msingi imara uwe na nyumba bora maisha yako yote.

Ni mimi rafiki yako na mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;
Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 (WhatsApp)
Blog: http://nyumbayakomaishayako.blogspot.com


      edit

5 comments:

  1. Replies
    1. Asante sana rafiki kwa kujifunza pamoja nasi maswala mbalimbali ya ujenzi! Kwa ushauri, maoni au maswali usisite kuwasiliana nami! Kila la kheri katika kuhakikisha unafikia ndoto zako za kuwa na nyumba bora kabisa!

      Delete
  2. Nashukuru Eng kwa elimu muhimu kwetu, ningependa kufahamu zaidi juu ya aina ya udongo na msingi unatakiwa kuwekwa kulingana na hali ya udongo....Natanguliza shukrani

    ReplyDelete
  3. Kati ya Moram au simenti kipi bora kwa msingi imara

    ReplyDelete
  4. Msingi eneo la kichanga Sana unatakiwa kutumia matofali au mawe, msaada mtaalamu

    ReplyDelete