Ujenzi wa majengo ni moja ya shughuli
ambazo zinafanyika kwa kasi katika maeneo mengi ya nchi yetu! Kufanya ujenzi ni
ndoto ya watu wengi na ni jambo zuri sana lakini watu wengi wamejikuta kwenye
matatizo mbalimbali kutokana na kukiuka ama kutokujua taratibu zinazohitajika kufwata kabla, wakati wa
ujenzi na baada ya ujenzi!
Ili kuepuka changamoto hizi leo nimeona
nikuandalie mambo muhimu unayohitaji kuyafahamu unapohitaji kibali cha ujenzi
wa majengo. Yafuatayo ni mambo matano ya msingi ya kuzingatia;
- Uwe na hati/udhibitisho wa umiliki wa kiwanja.
Hapa ni vizuri eneo lako
liwe kwenye ramani ya mipango miji yaani liwe limepimwa na umepewa hati miliki.
Eneo linapokuwa kwenye ramani ya mipango miji linakuwa limeainishwa matumizi
yake kama ni eneo la makazi, eneo la biashara, eneo la ibada, shule,,,, n.k Jambo hili ni la muhimu kwani ndio linakupa
msingi wa maamuzi ya aina ya jengo utakalojenga!
- Ubunifu wa Kitaalamu wa Jengo
Kutegemeana na aina ya
jengo hapa utahitaji kutafuta mtaalamu/wataalamu wa ujenzi (inaweza kuwa Msanifu
Majengo (Architect) au Mhandisi (Engineer)), ambao watakusaidia kufanya ubunifu
wa kitaalamu wa jengo lako kwa kuzingatia vigezo vyote vya eneo husika!
Unahitaji kuwa na jengo la kisasa, lenye mvuto, usalama wa kutosha na gharama
nafuu na hivi vyote unavipata kwenye ubunifu.
- Kujaza Fomu Serikali ya Mtaa
Kuna fomu maalumu za
kujaza kutoka serikali ya mtaa unakoishi kwa ajili ya kwenda kuombea kibali
halmashauri/ manispaa husika
- Kupeleka Michoro na Fomu ya Maombi Halmashauri/ Manispaa
Kutoka kwenye ubunifu
utapewa michoro mbalimbali inayoonyesha muonekano wa jengo lako kuanzia kwenye
msingi mpaka kwenye paa. Michoro hii utaambatanisha na fomu kutoka serikali ya
mtaa na kupeleka manispaa. Michoro yote inabidi iwe imepigwa mihuri na sahihi
ya mtaalamu wa ujenzi aliyesajiliwa. Hapa mtaalamu wako wa ujenzi anaweza
kukusaidia kupeleka michoro na kukufanyia mchakato wa kuomba kibali. Kwa upande
wa Architect huwa inapelekwa seti tatu za michoro na kwa upande wa Engineer
huwa inapelekwa seti mbili za michoro pamoja na ripoti ya mahesabu ya ubunifu
(Design Calculation Report).
- Gharama na Muda wa Kutoa Kibali
Ukishakabidhi michoro
manispaa husika kuna gharama kidogo ambazo utahitaji kulipia ili uweze kupata
kibali. Gharama hizi zinatofautiana baina ya jengo na jengo kuanzia kwenye
ukubwa wa jengo mpaka kwenye matumizi ya jengo husika. Ukifika manispaa michoro
itakaguliwa na kisha utakadiriwa gharama za kibali ambazo utalipia na kisha
utapewa risiti halafu hatua nyingine zitaendelea mpaka pale utakapopewa taarifa
kwamba kibali chako kimetoka ambapo kwa siku hizi haichukui muda mrefu sana
hasa kama jengo lako limefata vigezo vyote. Kwa mujibu wa kifungu cha 35 (i)
cha sharia ya mipangomiji No. 8 ya mwaka 2007, Mamlaka ya upangaji inatakiwa
kutoa kibali cha ujenzi katika kipindi kisichozidi SIKU 60 tangu mwombaji alipowasilisha maombi yake. Aidha ndani ya
kipindi hicho mamlaka inatakiwa kumtaarifu mwombaji kama amekubaliwa au
amekataliwa maombi yake na kutaja sababu zilizopelekea ombi lake kukataliwa.
Hizo ndio hatua muhimu rafiki ambazo
unahitaji kuzijua unapohitaji kibali cha ujenzi wa jengo lako! Usisite
kuwasiliana na mtaalamu wako wa ujenzi kwa usaidizi na maelekezo zaidi!
KUMBUKA: Kufanya ujenzi hasa wa jengo lolote kiholela bila kibali kunaweza kukuweka kwenye matatizo makubwa ikiwemo
kusimamishwa ujenzi na kupigwa faini ya fedha ambayo ni kubwa sana ukilinganisha
na gharama ambazo ungetumia wakati wa usajili. Unaweza kuepuka haya yote kwa
kuzingatia ushauri nilioelekeza hapo juu.
Asante sana kwa kuwa nami;
Jina: Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
0 comments:
Post a Comment