Moja ya jambo
ambalo limekuwa likinishangaza kwenye ujenzi wa nyumba ni jinsi ambavyo watu
wamekuwa wakipuuzia umuhimu wa ubunifu wa jengo kabla ya kuanza ujenzi. Wateja
wengi wamekuwa wakiniambia ubunifu (design) ni kwa ajili ya ujenzi wa miradi
mikubwa ya makampuni kitu ambacho si kweli hata kidogo. Jengo lolote (kuanzia
majengo madogo ya kuishi mpaka majengo makubwa ya kibiashara) ni lazima
kufanyiwa ubunifu wa kitaalamu ili kuhakikisha yanasimama imara na kuwa na
muonekano unaotakiwa.
Nilichogundua ni
kwamba watu wengi wana woga kuhusu gharama za ubunifu, baadhi ya wateja
wanasema gharama ni kubwa sana, na wengine hawajui hata kama ujenzi unahitaji
kuwa na mtaalamu wa ujenzi kwa ajili ya kufanya ubunifu.
Kuna mteta mmoja
niliwahi kukutana naye alikuwa anataka kujenga nyumba ya ghorofa ambayo kwa
haraka haraka gharama yake si chini ya Tshs mil 140 lakini alikuwa anataka
ramani ya laki mbili. Tena akawa ananiambia kuna ramani huko mtaani eti
zinauzwa kwa laki moja tu. Nilipomwambia aniletee hiyo ramani ya mtaani kwa bei
hiyo na mimi nilipomwonyesha ramani ya nyumba nyingine iliyokamilika ndipo
akagundua kuwa kinachouzwa mtaani ni sehemu ndogo sana sana ya kile
kinachotakiwa na hakina manufaa yoyote kwenye ujenzi wa nyumba. Rafiki yangu ni
muhimu kuwa makini sana maana siku hizi kumekuwa na matapeli wengi na taarifa
nyingi za uwongo ambazo ni rahisi kukupoteza
Hasara za kuepuka kufanya ubunifu.
Umewahi kusikia
jengo la ghorofa limedondoka? Umewahi kupita sehemu ukakuta nyumba ina mipasuko
kama tetemeko limepita wakati nyumba nyingine ziko vizuri? N,k Kama umewahi
kukutana na jengo ambalo limemalizika kujengwa halafu ndani ya muda mfupi
likaanza kuonyesha udhaifu kama mipasuko au kubomoka basi kuna uwezekano mkubwa
sana halikufanyiwa ubunifu yakinifu au wamenunua ramani sehemu na kuja kujenga
bila kumhusisha mtaalamu wa ujenzi. Hasara kubwa ya kuepuka kufanya ubunifu wa
ujenzi ni kupata jengo lisilokidhi viwango vya majenzi. Hasara nyingine kubwa
ni kutumia gharama nyingi kuliko gharama halisi zinazohitajika kwa ujenzi wa jengo
lako (Mbaya Zaidi ni kwamba utapoteza pesa nyingi na hutajua kama umepoteza
pesa hizo).
Je ni gharama kiasi gani zinahitajika kwenye ubunifu?
Kabla
sijakuambia gharama zinakuwaje rafiki yangu ngoja nikueleze kitu kimoja muhimu.
Hakuna kazi ngumu kama kazi ya kufikiria hasa katika zama hizi ambazo kuna
kelele nyingi sana. Na moja ya vitu vinavyohitaji ufikiri wa hali ya juu ni UBUNIFU. Unapompa mtaalamu wa ujenzi kazi ya kufanya
ubunifu unampa kazi ya kufikiri kwa kina namna ya kupangilia na kuhakikisha
uimara wa jengo lako kwa namna unavyotaka wewe na baada ya hapo akutengenezee
ramani ya nyumba hiyo ili uweze kuitumia kufanya ujenzi. Hili si jambo rahisi
hata kidogo hasa ukizingatia kila mteja ana matakwa yake ya tofauti kuhusu aina
ya nyumba anayotaka kuishi.
Kwa kuangalia
maelezo hayo hapo juu utagundua kuwa hakuna gharama moja ambayo inayoweza
kutumika kwa kila jengo, bali kila jengo litakuwa na gharama yake ya ubunifu
kulingana na mahitaji ya mteja. Jambo la kuzingatia ni kwamba kadiri mahitaji
ya nyumba yanavyokuwa mengi ndivyo gharama za ubunifu zinavyokuwa kubwa.
Kwa uzoefu wangu
wa kufanya ubunifu na kujenga majengo ya aina mbalimbali; gharama za ubunifu
huwa ni kati ya Tshs laki tano na TShs
mil 5 za kitanzania kutegemeana na mahitaji ya mteja. Kuna wakati inaweza
ikawa chini ya hapo au juu ya hapo, jambo la msingi ni kuhakikisha unamweleza
kwa kina mtaalamu wa ujenzi kuhusu kile unachokitaka ili aweze kukukadiria
gharama stahiki kwa jengo lako.
Hali ya
Kufikirisha
Bado kuna watu
utawasikia wakilalamika gharama hizo zipo juu. Hebu fikiria mtu unataka kujenga
nyumba yenye thamani ya Zaidi ya mil 90 lakini mtaalamu wa ujenzi anakufanyia
ubunifu kwa gharama labda ya Tshs mil 1.5; Hivi kweli utasema gharama ziko juu?
Epuka sana vitu vya bei rahisi rafiki hasa linapokuja swala la ujenzi maana nyumba ni
moja ya sehemu muhimu sana ya maisha yako hapa duniani.
Usijenge kwa
mazoea, Jenga kitaalamu Ili nyumba yako iwe na thamani siku zote.
Ni mimi rafiki
yako na mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;
Jina: Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
0 comments:
Post a Comment