T
|
unapoongelea maswala ya ujenzi mara nyingi watu tunawaza
zaidi jengo litakuwaje, namna vyumba vitakavyokaa, sebule, jiko, vyoo na mambo
mengine yatakayopatikana ndani ya nyumba. Wengi wetu tunapenda kuzama zaidi
kwenye mpangilio, ukubwa na uzuri wa jengo tu.
Leo rafiki yangu ngoja nikupe siri ya eneo jingine ambalo
nalo linaongeza thamani kubwa kwenye nyumba yako na kuifanya kuwa bora zaidi.
Eneo hili ni eneo ambalo wengi wetu tunalisahau mara nyingi na kujikuta
hatulitendei haki kabisa. Eneo hili si jingine bali ni ENEO LA NJE YA NYUMBA au
kwa kingereza tunaita “Exterior Landscaping”
Eneo la Nje ya Nyumba au Mandhari ya Nje ya nyumba yako ni
eneo ambalo linahitaji ubunifu wa hali ya juu. Ni eneo ambalo ukilitumia vizuri
linaboresha nyumba yako na ukilikosea linapoteza thamani ya nyumba yako kabisa
au kwa kiasi Fulani. Watu wengi wanashindwa kupangilia mandhari ya nje ya
nyumba kwa sababu wanajenga bila ushauri wa wataalamu. (Mfano mtu anachukua
ramani kwa rafiki au jirani anatafuta fundi na kuanza kujenga bila hata
kudadisi namna ramani hiyo itakavyokaa kwenye eneo lake). Mwisho wa siku
anajikuta ameshafanya maamuzi mabovu na hawezi kuyabadili. Usifanye kosa hilo
rafiki yangu.
Ubunifu wa eneo la Nje unafanyikaje?
Ubunifu wa mandhari ya nje ya nyumba mara nyingi unafanywa
wakati wa kutengeneza ramani ya jengo. Unapokubaliana na msanifu majengo
kukutengenezea ramani inabidi usisahau kuomba mpangilio wa eneo la nje. Mbunifu
itabidi aje kwenye eneo lako la ujenzi ili apate
vipimo vya eneo lako na kujua kama eneo lako lina mteremko au la ili aweze
kulipangilia vizuri. Hata kama umeshajenga nyumba yako na imekamilika bado
unaweza ukapata ushauri mzuri tu wa namna ya kuhakikisha unatengeneza eneo lako
la nje ya nyumba na kulifanya liwe bora kabisa.
Malighafi Zinazotumika Kutengeneza Eneo la Nje ya Nyumba
Eneo la nje ya nyumba linaweza kutengenezwa kwa kutumia
malighafi za aina nyingi sana. Unaweza ukachanganya mimea ya maua na miti
midogomidogo, unaweza ukatumia ukoka, miti ya matunda, maua ya kutengeneza
(plastiki) au unaweza ukatumia malighafi ngumu kama zege, tofali ngumu, tanga
stone, vigae, mbao, makuti, n.k… Unapotengeneza eneo lako Unaweza ukatumia
malighafi ya aina moja au ukachanganya kulingana na jinsi jengo na eneo lako
lilivyo.
Nini Faida za kuboresha Mandhari ya Nje ya Eneo lako?
Zifuatazo rafiki yangu ni faida chache kati ya nyingi sana
utakazopata kwa kuboresha mandhari ya eneo lako;
i.
Kuongeza uzuri au mvuto wa jengo lako tangu
unapoanza kuingia kwenye geti lako mpaka unapofika ndani ya nyumba yako.
ii.
Kupata sehemu nzuri ya kupumzika nje ya nyumba
yako.
iii.
Kupata hewa safi na mazingira safi ya kuishi
iv.
Kutunza nyumba na kuifanya idumu kwa muda mrefu
Gharama za kutengeneza mandhari ya nje zikoje?
Gharama zinategemeneana sana na ukubwa wa eneo lako na namna
ambavyo utapangilia eneo lako. Unaweza ukawa na bajeti ndogo tu lakini
ukafanikiwa kutengeneza kitu kizuri kabisa na chenye mvuto wa aina yake.
Unachotakiwa ni kumuomba mshauri wa ujenzi akupe machaguzi ambayo utayafanyia
kazi na kuona lipi linakufaa.
Kumbuka : Chochote unachotaka kwenye maisha yako unaweza
kukipata kama utaamua kwa dhati kuchukua hatua na kufanyia kazi ndoto zako.
#BoreshaMandhariYaJengo
#TumiaWataalamuWaUjenzi
#EpukaKufanyaMakosaYasiyoYaLazima
#OkoaGharamaZaUjenzi
Ni mimi rafiki yako na mhamasishaji katika maswala ya
ujenzi.
Eng Beatus B. Laswai
blog: nyumbayakomaishayako.blogspot.com
Mobile
: 0752 655 084 / 0782 129 412 / 0712 877 343
Email
: engbeatus.laswai@gmail.com
0 comments:
Post a Comment