Habari ya leo rafiki yangu mpendwa na mfatiliaji wa blogu
hii ya “Nyumba yako, Maisha yako”. Hongera sana kwa siku hii nyingine tulivu
kabisa ambapo tunaenda kufanya yaliyo bora na kutegemea kupata matokeo bora
kabisa.
Leo tuelimishane kidogo kuhusu udongo wa mfinyanzi! Udongo
wa mfinyanzi ni upi? Jinsi ya kutambua udongo wa mfinyanzi? Madhara yake kwenye
ujenzi….. Na namna bora ya kujenga kwenye udongo wa mfinyanzi!
Unapotaka kufanya ujenzi kitu cha kwanza na cha muhimu ni
kutambua aina ya udongo uliopo kwenye eneo lako la ujenzi. Utambuzi huu
utakusaidia kujua namna ya kufanya ujenzi wako ili kuepuka changamoto za
kufanya marekebisho mengi baada ya ujenzi kukamilika. Kama hujui aina za udongo
ni vyema ukawasiliana na mtaalamu wa ujenzi akueleze kwa kina kuhusu aina na
tabia za udongo kulingana na mahali ulipo.
Jinsi ya Kutambua Udongo wa Mfinyanzi
Udongo wa mfinyanzi ni udongo wenye tabia ya kusinyaa na
kutanuka. Kukiwa na unyevu unyevu udongo huu hutanuka na endapo unyevunyevu
utapungua au kukauka udongo huu husinyaa na kuacha nafasi (kupasuka pasuka).
Tabia hii husababisha nguvu ya msukumo inayokinzana ambayo itasababisha madhara
endapo utafanya ujenzi kwenye udongo huu bila kuzingatia kanuni za ujenzi
kwenye eneo la mfinyanzi.
Njia rahisi ya kutambua udongo wa mfinyanzi ni kuangalia
alama za mipasuko kwenye ardhi. Mipasuko hii hutokea hasa kipindi cha kiangazi
ambapo udongo huu unasinyaa sana kutokana na kutokuwa na unyevunyevu.
*Athari za udongo huu kwenye nyumba yako*
Udongo wa mfinyanzi unaposinyaa unakuwa na hatari zaidi
kwenye nyumba yako kuliko unapotanuka. Kama tulivyoona hapo juu udongo huu
ukisinyaa unakuwa na mipasuko inayoacha nafasi hali inayosababisha nguvu kubwa
ya mvutano kwenye msingi wa nyumba. Hali hii inapotokea nyumba yako itapata
nyufa au mipasuko (cracks) kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo msingi, kuta,
nguzo, sakafu, tiles, beam pamoja na maeneo mengine. Hali hii ya mipasuko
huharibu taswira ya jengo na kulifanya liwe hatari kwa matumizi. Jengo lenye
shida hii litahitaji marekebisho ya mara kwa mara ili kuziba nyufa na kubadili
sehemu zilizoharibika na wakati mwingine inakuwa ngumu kabisa kuishi kwenye
nyumba ya namna hii kitu ambacho ni hasara kubwa kwa mmiliki wa jengo.
Mfano wa mpasuko kwenye nyumba kutokana na nguvu kubwa ya
mvutano kwenye udongo
*Hatua za Kuchukua Unapotaka Kufanya Ujenzi kwenye Eneo lenye Udongo wa Mfinyanzi*
Kuna njia mbalimali za kufanya ujenzi kwenye mfinyanzi lakini leo nitaongelea njia kuu mbili unazoweza kuzitumia kupambana na udongo wa aina hii;
1. Kuondoa kabisa udongo wa mfinyanzi eneo utakalojenga msingi
1. Kuondoa kabisa udongo wa mfinyanzi eneo utakalojenga msingi
Mbinu hii inatumika ili kuhakikisha msingi
wako haugusani kabisa na udongo wa mfinyanzi. Ukishaondoa udongo wa mfinyanzi
unaleta udongo mwingine mpya na kuuweka kwenye eneo husika ambapo utajenga
msingi wako. Njia hii inaweza ikaonekana ina gharama kubwa wakati unaanza
ujenzi lakini ni njia ya uhakika kuhakikisha hautakutana na changamoto za
mipasuko baada ya kumaliza ujenzi. Kwa kutumia mtaalamu wa ujenzi utashauriwa
namna ya kutoa udongo uliopo na kuweka mwingine kwa kiasi kinachotakiwa na kwa
gharama nafuu.
2. Kuhakikisha maji hayafikii eneo ulilojenga msingi wako
Ili udongo wa mfinyanzi utanuke na kusinyaa
unahitaji maji (unyevunyevu). Unaweza ukajenga nyumba yako bila kuondoa udongo
wote wa mfinyanzi (na hapa inashauriwa ujenge kipindi cha kiangazi ambapo
udongo unakuwa umesinyaa) halafu ukimaliza ujenzi unaweka miundombinu ambayo
utahakikisha maji hayafiki kwenye msingi wa nyumba yako. Njia hiii inaweza
ikaonekana rahisi lakini hugeuka kuwa ya gharama kubwa hasa kipindi cha mvua
ambapo utatakiwa kuhakikisha maji yote yaliyopo na yanayokuja kwenye eneo lako
unayatafutia uelekeo wa tofauti ili yasizuru nyumba yako.
Mpaka kufikia hapo ndugu msomaji naamini umepata picha juu
ya ujenzi wa nyumba yako kama eneo lako lina udongo wa mfinyanzi na namna bora
ya kupambana na changamoto hiyo. Kwa maelezo na ushauri zaidi usisite
kuwasiliana na mtaalamu wako wa ujenzi.
Kumbuka
Sio kila mpasuko au nyufa kwenye nyumba yako umesababishwa
na udongo wa mfinyanzi, kwenye ujenzi kuna changamoto nyingi sana hivyo kama
hujajenga nyumba yako kwenye udongo wa mfinyanzi na imetokea ina mipasuko basi
ni muda muafaka wa kumtafuta mtaalamu wa ujenzi ili akushauri tatizo ni nini na
namna bora ya kulitatua.
Jenga Kitaalamu, Jifunze Mbinu Bora za Ujenzi, Ishi Maisha
ya Furaha na Yenye Thamani.
Rafiki yako mpendwa
Eng Beatus B. Laswai
Mobile
: 0752 655 084
Email
: engbeatus.laswai@gmail.com
Asante Sana kwa ushauri.
ReplyDeleteKaribu sana rafiki!
Delete