Habari ya leo rafiki yangu mpendwa na mfatiliaji wa blogu hii ya “Nyumba yako, Maisha yako”. Hongera sana kwa siku hii njema kabisa ambapo tunaenda kufanya yaliyo bora na kutegemea kupata matokeo bora kabisa.
Leo karibu tujifunze namna ya kutambua eneo bora linalofaa
kwa ujenzi wa nyumba yako iwe ni ya makazi ama biashara. Unapofanikiwa kujenga
katika eneo zuri linalokidhi mahitaji yako unaipa nyumba yako thamani kubwa na
kuifanya iendelee kuwa na thamani hiyo kwa miaka mingi ijayo. Utambuzi wa eneo
bora na zuri la ujenzi unazingatia mambo makuu matatu muhimu.
1. Jambo la Kwanza ni Usalama
Hili ni jambo muhimu sana la kuangalia unapokuwa unatafuta eneo la
kufanya ujenzi wa nyumba yako. Linapokuja swala la usalama kuna vitu vingi sana
vya kuangalia na leo nitakuorodheshea baadhi ya vitu hivyo;
i.
Je eneo lako halipo kwenye mkondo wa maji? Tafadhali
usijenge kwenye eneo lenye mkondo wa maji kwa sababu unakuwa kwenye hatari
kubwa ya kupatwa na mafuriko pamoja na changamoto nyingine za kujenga eneo lenye maji hasa yanayotembea.
ii. Je hakuna upepo mkali? Unapotaka kujenga hasa kama eneo lako lipo
sehemu ya wazi sana lazima ujitahidi upate taarifa za eneo hilo kuhusu upepo
mkali ama uwepo wa vimbunga. Taarifa hizi zitakupa mwongozo sahihi kabla
hujaanza ujenzi.
iii.
Uwepo wa wanyama wakali. Kama unafanya ujenzi
maeneo ya nje ya mji au eneo ambalo palikuwa na pori au karibu na mbuga ya
wanyama lazima upate taarifa za mwingiliano wa wanyama hatarishi na binadamu.
Kama kuna ripoti za watu kushambuliwa ni vizuri kuepuka maeneo hayo
iv. Aina ya udongo katika eneo husika. Hili ni
muhimu katika kuhakikisha jengo lako linasimama sehemu imara na kuepuka
kuporomoka wakati wa ujenzi au baada ya ujenzi kukamilika. Katika hili na
mengine mengi utahitaji mtaalamu wa ujenzi ili kukushauri hatua muhimu za
kuchukua.
v. Uwepo wa kemikali au vimiminika vya hatari
kwenye udongo. Kama eneo lako lipo karibu na viwanda vya kemikali hatari ni
vizuri kupima udongo wa eneo hilo ili kujua kama kuna kiwango hatarishi cha
kemikali ambacho kinaweza kuwadhuru wale wote watakaoishi kwenye nyumba
unayotarajia kujenga.
Listi ni ndefu kwakweli ila kwa leo
naomba niishie hapo. Chamsingi inabidi utambue vitu hivi ni muhimu sana na
taarifa zake ni rahisi kupatikana endapo utaamua kuzitafuta.
2. Jambo la Pili ni Namna ya Kufika kwenye Eneo Lako.
Swali la msingi hapa ni je eneo lako linafikika kirahisi? Ufikikaji
katika eneo lako unaathari kubwa sana kwenye gharama za ujenzi wa nyumba yako.
Kama eneo lipo mbali na malighafi za ujenzi kiasi kwamba haziwezi kufika
kirahisi kwenye eneo lako basi inabidi ujue hali hii itasababisha gharama za
ujenzi ziwe juu sana. Mbali na malighafi za ujenzi inabidi pia uangalie
upatikanaji wa mafundi pamoja na mahitaji mengine muhimu ya binadamu kama chakula na malazi wakati wa
ujenzi na baada ya ujenzi kukamilika. Njia nzuri ya kuchunguza hili ni
kuangalia umbali utakaotembea kwa mguu kupata mahitaji ya msingi.
Mbali na hicho tulichoona hapo juu eneo lako linaweza likawa mjini kabisa
lakini bado likawa halifikiki kirahisi na hivyo kutokidhi mahitaji yako.
Maswali ya kujiuliza kuhusiana na swala hili ni kama yafuatayo; Je kuna foleni
kiasi gani kuelekea eneo unaloishi? Je watoto wako ungependa wasome shule zipi
kutoka hapo ulipo? Je sehemu kama hospitali, super markets, migahawa, masoko,
vituo vya mafuta (Petrol stations) vinafikika kwa urahisi kiasi gani? Je
marafiki zako na familia yako wanaishi umbali gani toka ulipo? Je vitu
unavyovipenda (hobbies) vinapatikana kwa urahisi kiasi gani?
Haya ni baadhi ya maswali muhimu sana ambayo yatakupa mwanga wa kufanya
maamuzi ya wapi ujenge ili kukidhi mahitaji yako.
Unaweza Kusoma Pia: Kwanini ni Muhimu Kufanya Ujenzi Kwenye Eneo Lililorasimishwa!
3. Swala la tatu ni Ukubwa wa kiwanja na matumizi ya eneo unalotaka kujenga
Hili
ni swala ambalo watu wengi hawalipi umakini wa kutosha na hivyo kujikuta
wakijenga bila kufuata kanuni za ujenzi. Ni lazima uongee na mtaalamu wa ujenzi
ili akusaidie kujua ukubwa wa eneo lako ukilinganisha na eneo la kiwanja (kwa
kingereza wanaita “Plot Ratio”). Unapokuwa na ufahamu wa ukubwa wa jengo lako
ukilinganisha na kiwanja chako pamoja na matumizi sahihi ya eneo lako unakuwa
umejihakikishia ujenzi bora kabisa na kuepuka usumbufu wa aina yoyote wakati wa
ujenzi au baada ya ujenzi kukamilika. Kuna watu wananunua kiwanja eneo la
msongamano (high density area) lakini wanataka kujenga kama wapo kwenye “Low
density area”. Tambua hitaji lako la
ujenzi mapema ili uweze kununua eneo sahihi litakaloendana na matumizi yako.
Linapokuja swala la ujenzi kila mtu ana vionjo vyake
anavyovitaka ambavyo vitamsaidia katika utambuzi wa eneo sahihi kwa ujenzi
wake. Mambo niliyokushirikisha hapo juu ni kwa ajili ya kukupa mwanga ili
ufanye maamuzi sahihi kabla hujaanza ujenzi wa nyumba yako. Sote tunatambua
nyumba bora iliyojengwa kwenye mazingira mazuri inachangia kwa kiasi kikubwa
katika kuboresha maisha ya wale watakaoishi ndani ya nyumba hiyo.
Cha msingi kabla hujaanza ujenzi wako ni vyema ukatafuta
washauri wa ujenzi (anaweza akawa msanifu majengo (Architect) au Mhandisi (Engineer))
ili uweze kupata ushauri sahihi kuhusiana na aina ya ujenzi unayotaka kufanya.
Kwa sasa nchi yetu ina wahandisi/wasanifu wengi ambao wanaweza kukushauri bure
kabisa au kwa gharama ndogo sana hivyo ni jukumu lako kuwatafuta.
Chukua hatua leo rafiki kwa kuhakikisha unapata eneo
linalokidhi mahitaji yako ili uweze kufanya ujenzi katika namna ambayo
itarahisisha maisha yako na kuyafanya yazidi kuwa bora Zaidi.
Rafiki yako mpendwa katika ujenzi wa taifa bora
Eng Beatus B. Laswai
Kwa maswali na ushauri kuhusu maswala ya ujenzi usisite kuwasiliana nami;
Namba: 0752 655 084 / 0782 129 412
Email: engbeatus.laswai@gmail.com
nyumbayakomaishayako.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment