Kuwa na taarifa sahihi za ujenzi kabla na
wakati wa ujenzi ni jambo la muhimu sana katika zama hizi kwa yeyote yule
anayefikiria kujishughulisha na shughuli za ujenzi. Tumekuwa tukiona watu mbalimbali
wakiingia kwenye matatizo ya kubomolewa nyumba zao na wengine wakipoteza ardhi
wanazomiliki au kuingia kwenye migogoro isiyoisha kutokana na kukosa taarifa na
maarifa sahihi kabla ya kufanya ujenzi.
Rafiki yangu mpendwa, kama unafikiria
kufanya shughuli yeyote ya ujenzi; Moja ya vitu muhimu kabisa vya kuzingatia
kabla hujaanza ujenzi ni kujua kama eneo unalotaka kujenga limepimwa au
halijapimwa. Na hapa ndipo tunaenda kujadili kwa kina ambapo tutaangalia mambo
matatu muhimu;
- Tofauti kati ya Kiwanja kilichopimwa (Surveyed Plot) na ambacho hakijapimwa (Unsurveyed plot)
- Faida ya Kufanya ujenzi kwenye kiwanja Kilichopimwa
- Hasara za kufanya ujenzi kwenye kiwanja ambacho hakijapimwa
*Tuanze moja kwa moja na tofauti baina ya
kiwanja kilichopimwa na ambacho hakijapimwa.*
Kiwanja kilichopimwa ni kile ambacho kina
hati na kinaonyesha mmiliki halali wa eneo hilo iwe ni kwa mauziano, kwa
kurithi au hata kwa kupewa zawadi. Eneo hili linakuwa limeonyeshwa kwenye
ramani ya mipango miji ambapo inakuwa imeonywesha ukubwa wa eneo kwa vipimo
halisi pamoja na matumizi sahihi ya eneo husika kulingana na mahitaji ya
mipango miji. Utalitambua eneo hili kwa kuangalia alama za mawe yaliyowekwa
kwenye kona za kiwanja.
Kwa upande wa pili, kiwanja kisichopimwa ni kile ambacho hakina
hati. Mara nyingi haya ni maeneo ambayo yanakuwa nje ya miji na yanakuwa chini
ya usimamizi wa halmashauri za vijiji. Maeneo haya yanakuwa hayana ramani rasmi
ya mipango miji na hivyo huwa hakuna mpangilio rasmi wa matumizi ya maeneo
haya.
*Pili tuangalie faida za kufanya ujenzi
kwenye eneo lililopimwa*
Baada ya kuona tofauti ya kiwanja kilichopimwa na ambacho hakijapimwa, zifuatazo ni faida chache kati ya nyingi
utakazozipata kwa kujenga kwenye kiwanja kilichopimwa
- Matumizi ya eneo yanakuwa yameainishwa waziwazi kwa mfano kama ni eneo la makazi, eneo la viwanda, eneo la kanisa/msikiti au eneo la biashara. kwa namna hii ni rahisi kujenga nyumba inayoendana na matumizi ya eneo
- Maeneo yaliyopimwa kunakuwa na huduma zote za kijamii kuanzia kwenye barabara, maji, maduka, maeneo ya wazi n.k
- Kutambulika rasmi na serikali kwa uwepo wako kwenye eneo husika na hivyo kuepuka migogoro na changamoto zisizo za lazima.
*Tatu tuangalie hasara za kufanya ujenzi
kwenye eneo ambalo halijapimwa..**
Unapojenga kwenye eneo ambalo halijapimwa
unakuwa umejiweka kwenye hatari zifuatazo
- Kutokuwa na uhakika wa matumizi ya eneo husika hali ambayo inaweza kusababisha ujikute unajenga nyumba ya makazi kwenye eneo la viwanda
- Uwezekano wa kupoteza nyumba yako pale ramani ya mipango miji itakapotoka na kuonyesha kwamba sehemu uliyojenga inahitajika itumike kwa matumizi mengine.
- Usumbufu mkubwa wa kuhamishwa kwenye eneo lako na kupewa sehemu nyingine au kulipwa fidia ya kuondoka kwenye eneo lako
Ndugu msomaji hayo ni mambo machache kati
ya mengi ambayo unapaswa kuyajua linapokuja swala la kiwanja kilichopimwa au
ambacho hakijapimwa. Kabla hujaanza ujenzi wako ni vyema ukajiridhisha kwa 100%
kwamba unajenga sehemu sahihi ambapo hutategemea kupata usumbufu labda itokee
majanga ya asili.
*Ushauri wangu kwako*
Kwa wale wenye maeneo ambayo hayajapimwa ni
vyema wakachukua hatua stahiki za kwenda manispaa kuomba ramani ya mipango miji
ili waweze kujua kuhusu mpangilio wa maeneo yao. Endapo itatokea manispaa
hakuna ramani ya mipango miji basi inabidi waombe kupimiwa maeneo hayo kabla
hawajaanza kuyaendeleza na hata kama wameshayaendeleza basi waombe ufanyike urasimishaji wa maeneo hayo ili waweze kutambulika rasmi kama wamiliki halali. Kwa kuwa gharama za upimaji zinaweza kuwa juu kama
ukiwa peke yako,, basi nashauri pia watu wenye maeneo yaliyo karibu karibu na
hayajipwa wajikusanye pamoja na kwenda kuomba upimaji ili kupunguza gharama
hizo.
Mbali na hayo niliyokueleza hapo juu kumbuka pia kuwasiliana na mshauri /
mtaalamu wako wa ujenzi ili aweze kukushauri na kukusaidia katika kufuatilia
baadhi ya vitu muhimu kabla ya kuanza ujenzi wako.
Muhimu zaidi tuhakikishe tunajenga katika maeneo
yaliyoainishwa vizuri ili kuepuka usumbufu kwa siku za mbeleni. Pia kwenye kununua ardhi tukumbuke kuna matapeli ambao wanaweza kukuingiza hasara mara mbili.
Nikutakie kila
la kheri katika kuhakikisha unakuwa na nyumba bora ya kuishi iliyojengwa katika
sehemu bora kabisa.
Rafiki yako mpendwa katika ujenzi wa taifa
bora
Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084
Email:engbeatus.laswai@gmail.com
0 comments:
Post a Comment