Nyumba
Bora ni Ipi?
Rafiki yangu mpendwa, moja ya hitaji muhimu sana kwa binadamu
yeyote yule ni kuwa na Makazi (Nyumba bora) kwa ajili yake pamoja na familia
yake. Pamoja na umuhimu huu mkubwa wa nyumba, bado watu wengi hawajatilia mkazo
katika kuhakikisha wanapata nyumba bora na mazingira bora ya kuishi. Katika
maeneo mengi ya nchi yetu ujenzi wa kiholela usiofata taratibu umekuwa ni jambo
la kawaida kitu ambacho kinasababisha watu kuishi kwenye miundo mbinu mibovu
kabisa.
Siku ya leo hebu tutafakari….. Ukisikia
neno “Nyumba Bora” kichwani mwako unapata picha gani? Je ni kitu gani kila mtu
anayefikiria kufanya ujenzi anatakiwa afanye ili aweze kuwa na nyumba bora?
Hebu tuanze na hili la *Nyumba Bora*;
Kwa kifupi, Nyumba bora ni ile ambayo
inakidhi mahitaji ya mteja (mwenye nyumba), Iliyojengwa kwa kufuata taratibu na
sheria za majenzi na ambayo ipo kwenye mazingira safi, tulivu na salama.
Zifuatazo ni sifa ambazo kwa pamoja zinasaidia katika kuwa na nyumba bora;
- Kufanya ujenzi katika eneo linalokubalika kisheria.
Kuna baadhi ya maeneo huwa yanatengwa kwa ajili ya
shughuli maalumu kama vile maeneo ya wazi, maeneo ya viwanda n,k. Hata ujenge
nyumba nzuri kiasi gani kama imejengwa eneo ambalo halikubaliki kisheria
unakuwa umepoteza thamani ya kuwa na nyumba bora maana muda wowote unaweza
kuingia kwenye changamoto ya kubomolewa na kuondolewa kwenye eneo hilo.
- Kufata ushauri wa wataalamu wa ujenzi.
Nyumba nyingi zinapoteza ubora na thamani wakati wa
ujenzi kutokana na kujengwa chini ya kiwango. Nyumba bora ni ile ambayo imezingatia
na kufata ushauri wa mtaalamu wa ujenzi kwa kuzingatia mahitaji ya mteja na
sehemu nyumba inapojengwa. Hata kama unajenga nyumba ndogo kiasi gani ni vizuri
ukahusisha mtaalamu wa ujenzi angalau kukupa ushauri na kukupa mwanga ufanye
nini.
- Upatikanaji wa mahitaji muhimu ya binadamu.
Nyumba yako ili iwe bora lazima iwe inafikika kiurahisi,
iwe karibu na huduma za kijamii, iwe na uwezekano wa kupata huduma za maji,
umeme na mahitaji mengine muhimu ikiwemo huduma za kiusalama.
- Matunzo / Usafi wa nje na ndani
Hili ni eneo ambalo watu wengi hasa maeneo ya mijini hawalitilikii
mkazo sana. unakuta watu wamezungukwa na uchafu, rangi ya nyumba inabanduka,
mabomba yanavuja na mambo mengine madogo madogo lakini hawajali. Unapoishi
mazingira yenye uchafu unajiweka katika hatari ya magonjwa, rangi ya nyumba
kubanduka kunasababisha kupoteza mvuto wa nyumba, maji maji kutokana na mabomba
kuvuja inaweza kuleta shida kwenye mhimili wa jengo. Ili nyumba yako iwe bora
ni lazima uijali na kuitunza ili isikuingize kwenye gharama zinazoweza
kuzuilika.
*Je ufanye nn ili uweze kuwa na nyumba bora? *
Baada ya kujua sifa za nyumba bora, kinachofata ni kuchukua hatua
sahihi ili uweze kumiliki kitu kilicho bora kabisa. Ukifuata ushauri ufuatao
utakuwa umejiwekea misingi imara ya kuhakikisha unakuwa na nyumba bora ya
kuishi ambayo utaipenda na kuifurahia kila wakati;
- Kwa wale ambao hawajaanza ujenzi wa nyumba; jambo la kwanza weka malengo sahihi kuhusu aina ya nyumba unayoitaka na lini hasa unaitaka. Lazima ujue kwa hakika ni aina gani ya nyumba unahitaji (Hapa unaweze kushauriana na mtaalamu wako wa ujenzi na ukapata wazo bora kabisa). Watu wengi wanashindwa kuwa na nyumba bora kwa sababu hawaweki lengo maalumu na mwisho wa siku wanajikuta wanafanya ujenzi ghafla ghafla tena kwa mazoea.
- Jambo la pili ni kuchukua hatua na hatua muhimu hapa ni kuanza kuwekeza kwa ajili ya nyumba yako. Anza na kiwango kidogo kabisa huku ukijipa hamasa kila siku. Usikurupuke tu na kuanza kujenga nyumba kwa kutumia fedha za mshahara au biashara. Nyumba ya kuishi kama tulivyoona kwenye kitabu cha “”Rich Dad Poor Dad”” ni Liability (inakuondolea pesa mfukoni) hivyo ni muhimu uwe na account maalumu ili usije ukaingia kwenye madeni au kusababisha kuyumba kwa biashara.
- Tafuta mtaalamu wa ujenzi kwa ajili ya kupata ushauri na kutengeneza picha ya jengo lako. Siku hizi kuna mbinu nyingi na mpya za ujenzi ambazo zinaweza kukusaidia katika kupata nyumba bora kwa gharama nafuu kabisa. Mtaalamu wa ujenzi akishajua mahitaji yako ni rahisi kukushauri njia sahihi ya kuchukua ili ufikie lengo lako. Hapa utapata elimu sahihi kuhusu matumizi ya kiwanja chako, sharia za majenzi, nini ufanye kabla ya ujenzi, wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi.
- Anza Sasa. Ukitaka uzuri sharti uzurike; ukitaka nyumba bora inabidi ujitoe kwelikweli na usisubiri mpaka mambo yakae vizuri ndo uanze, ANZA SASA. Kinachowafanya watu wengi kujenga nyumba zisizo na ubora ni kufanya ujenzi kwa pressure bila kuwa na mpangilio maalumu.
Kuwa na nyumba bora utakayoifurahia muda
wote ni jambo linalowezekana kabisa.
Kwa ushauri, maoni au maswali usisite kuwasiliana nami……
Jina: Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
0 comments:
Post a Comment