Habari ya leo rafiki yangu na
mfatiliaji wa blogu hii nzuri kabisa ya “Nyumba Yako, Maisha Yako”. Nina Imani
unaendelea kupambana vilivyo kuhakikisha unafanya dunia kuwa mahala salama na
bora kabisa kuishi. Leo rafiki yangu karibu tujifunze kuhusu aina za vyoo
ambavyo ni maalumu kwa ajili ya wazee, walemavu na watoto. Aina hizi za vyoo
hazina utofauti sana na aina nyingine za kawaida bali zinakuwa zimefanyiwa
maboresho kidogo ili kukidhi mahitaji ya makundi haya. Hivyo Kama unategemea
kuishi na mzee au mlemavu au mtoto usijiumize kichwa sana, karibu tujifunze
namna ya kuwasaidia kupata huduma bora kabisa ya choo.
Choo kwa Ajili Ya Wazee/Walemavu
Boresho la kwanza ni kuweka
sehemu ya kujishikiza ili kuwapa ufanisi wazee na walemavu wakati wanapotaka kukaa na wakati wa
kuondoka baada ya kujisaidia. Sehemu hii ya kujishikiza inaweza ikatengenezwa
ukutani karibu na choo kilipo au ikashikizwa kabisa kwenye choo.
Boresho la pili ni kuongeza urefu
wa sehemu ya choo cha kukaa mpaka kufikia angalau 75cm. Choo cha kawaida kina
urefu wa 50cm – 55cm. Urefu huu umeongezwa ili kuwapa urahisi wa kukaa bila
kukunja miguu sana na hivyo kuwa na nguvu za kutosha wakati wa kuinuka baada ya
kujisaidia.
Kwa kuzingatia maboresho haya
mawili, mzee au mlemavu anaweza kujisaidia bila shida yoyote. Unapoanza ujenzi
wa nyumba yako ni vyema ukakumbuka kuhusu hitaji hili la muhimu kabisa ili
kuhakikisha unaandaa mazingira bora kwa ajili ya watu wa makundi yote.
Choo kwa Ajili Ya Watoto
Inashauriwa kutumia Zaidi vyoo
vya kuchuchumaa kwa ajili ya watoto ili waweze kujisafisha vizuri na kujiepusha
na hatari za magonjwa.
Choo cha watoto ni muhimu sana
hasa kama unataka kuwajengea watoto utamaduni wa kujisaidia katika mazingira
mazuri. Ubunifu huu unaweza ukafanyika sehemu mbalimbali kuanzia majumbani, hospitalini, kwenye mahoteli pamoja na sehemu nyingine.
Mpaka hapo rafiki yangu naamini
kuna kitu kizuri umeweza kujifunza hasa kwa kutambua kwamba kuna namna bora
kabisa ya kuhakikisha wazee, walemavu na watoto wanapata huduma bora ya choo.
Hivyo utakapokuwa unafanya ujenzi ni vyema ukakumbuka elimu hii na kuifanyia
kazi.
Ni mimi rafiki yako na
mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;
Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 (WhatsApp)
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
Blog: nyumbayakomaishayako.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment