Published July 29, 2018 by with 0 comment

Ongeza Uzuri wa Nyumba kwa Kutengeneza Mandhari ya Nje ya Nyumba (Exterior Landscaping)


T
unapoongelea maswala ya ujenzi mara nyingi watu tunawaza zaidi jengo litakuwaje, namna vyumba vitakavyokaa, sebule, jiko, vyoo na mambo mengine yatakayopatikana ndani ya nyumba. Wengi wetu tunapenda kuzama zaidi kwenye mpangilio, ukubwa na uzuri wa jengo tu.
Leo rafiki yangu ngoja nikupe siri ya eneo jingine ambalo nalo linaongeza thamani kubwa kwenye nyumba yako na kuifanya kuwa bora zaidi. Eneo hili ni eneo ambalo wengi wetu tunalisahau mara nyingi na kujikuta hatulitendei haki kabisa. Eneo hili si jingine bali ni ENEO LA NJE YA NYUMBA au kwa kingereza tunaita “Exterior Landscaping”

Eneo la Nje ya Nyumba au Mandhari ya Nje ya nyumba yako ni eneo ambalo linahitaji ubunifu wa hali ya juu. Ni eneo ambalo ukilitumia vizuri linaboresha nyumba yako na ukilikosea linapoteza thamani ya nyumba yako kabisa au kwa kiasi Fulani. Watu wengi wanashindwa kupangilia mandhari ya nje ya nyumba kwa sababu wanajenga bila ushauri wa wataalamu. (Mfano mtu anachukua ramani kwa rafiki au jirani anatafuta fundi na kuanza kujenga bila hata kudadisi namna ramani hiyo itakavyokaa kwenye eneo lake). Mwisho wa siku anajikuta ameshafanya maamuzi mabovu na hawezi kuyabadili. Usifanye kosa hilo rafiki yangu.

 

Ubunifu wa eneo la Nje unafanyikaje?

Ubunifu wa mandhari ya nje ya nyumba mara nyingi unafanywa wakati wa kutengeneza ramani ya jengo. Unapokubaliana na msanifu majengo kukutengenezea ramani inabidi usisahau kuomba mpangilio wa eneo la nje. Mbunifu itabidi aje kwenye eneo lako la ujenzi ili apate vipimo vya eneo lako na kujua kama eneo lako lina mteremko au la ili aweze kulipangilia vizuri. Hata kama umeshajenga nyumba yako na imekamilika bado unaweza ukapata ushauri mzuri tu wa namna ya kuhakikisha unatengeneza eneo lako la nje ya nyumba na kulifanya liwe bora kabisa.

Malighafi Zinazotumika Kutengeneza Eneo la Nje ya Nyumba

Eneo la nje ya nyumba linaweza kutengenezwa kwa kutumia malighafi za aina nyingi sana. Unaweza ukachanganya mimea ya maua na miti midogomidogo, unaweza ukatumia ukoka, miti ya matunda, maua ya kutengeneza (plastiki) au unaweza ukatumia malighafi ngumu kama zege, tofali ngumu, tanga stone, vigae, mbao, makuti, n.k… Unapotengeneza eneo lako Unaweza ukatumia malighafi ya aina moja au ukachanganya kulingana na jinsi jengo na eneo lako lilivyo.

Nini Faida za kuboresha Mandhari ya Nje ya Eneo lako?

Zifuatazo rafiki yangu ni faida chache kati ya nyingi sana utakazopata kwa kuboresha mandhari ya eneo lako;
i.                     Kuongeza uzuri au mvuto wa jengo lako tangu unapoanza kuingia kwenye geti lako  mpaka unapofika ndani ya nyumba yako.
ii.                   Kupata sehemu nzuri ya kupumzika nje ya nyumba yako.
iii.                  Kupata hewa safi na mazingira safi ya kuishi
iv.                  Kutunza nyumba na kuifanya idumu kwa muda mrefu

Gharama za kutengeneza mandhari ya nje zikoje?

Gharama zinategemeneana sana na ukubwa wa eneo lako na namna ambavyo utapangilia eneo lako. Unaweza ukawa na bajeti ndogo tu lakini ukafanikiwa kutengeneza kitu kizuri kabisa na chenye mvuto wa aina yake. Unachotakiwa ni kumuomba mshauri wa ujenzi akupe machaguzi ambayo utayafanyia kazi na kuona lipi linakufaa.

Kumbuka : Chochote unachotaka kwenye maisha yako unaweza kukipata kama utaamua kwa dhati kuchukua hatua na kufanyia kazi ndoto zako.

#BoreshaMandhariYaJengo
#TumiaWataalamuWaUjenzi
#EpukaKufanyaMakosaYasiyoYaLazima
#OkoaGharamaZaUjenzi
 


Ni mimi rafiki yako na mhamasishaji katika maswala ya ujenzi.
Eng Beatus B. Laswai
blog: nyumbayakomaishayako.blogspot.com
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412 / 0712 877 343
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
                                                                        
Read More
      edit