Published April 01, 2019 by with 5 comments

Msingi Imara, Nyumba Imara




Moja ya maamuzi mabovu kabisa ambayo hutakiwi kuyafanya linapokuja swala la ujenzi wa nyumba yako ni kutokujenga msingi imara. Ngoja nikupe mfano rafiki; Mmoja wa marafiki zangu wakati nasimamia ujenzi wa nyumba yake maeneo ya Iringa; majirani zake walikuwa wanamwambia tunatumia gharama kubwa sana kwenye msingi kama vile tunajenga ghorofa mpaka ikafika wakati akawa anahisi kama vile anapoteza pesa ya bure. Miezi kadhaa baada ya nyumba yake kukamilika ndipo alipoona umuhimu wa kile tulichokifanya  kwani ilikuwa kipindi cha mvua na nyumba za majirani zake karibu zote zilionyesha mipasuko (cracks). Walichosahau majirani zake ni kwamba eneo lile lina udongo wa mfinyanzi ingawa ulikuwa kwa kiasi kidogo na hivyo ilitakiwa waweke msingi imara kabisa.

Leo rafiki yangu napenda kukushirikisha umuhimu wa kuwa na msingi imara. Utaweza kufahamu msingi imara ni upi na ni kwa namna gani utahakikisha unakuwa na msingi imara kabisa ili ujihakikishie ujenzi wa nyumba bora.



*Msingi Imara* kwa ufupi ni ule ambao unaweza kuhimili uzito wa jengo pamoja na nguvu kutoka nje kama vile upepo, msukumo wa udongo, mitikisiko pamoja na nguvu nyingine za asili. Msingi huu unaweza ukajengwa kwa kutumia mawe, matofali ya block, Zege au malighafi nyingine ambazo zinakubalika kwenye ujenzi. Unapokuwa na msingi imara unajihakikishia usalama wako, mali zako na wote watakaoishi ndani ya nyumba yako na pia utaweza kujikinga kwa namna Fulani na majanga ya asili kama vile matetemeko na mitikisiko ya ardhi.

SOMA HAPA: Hatua Tatu Muhimu Ujenzi wa Msingi Imara

*Namna ya kuhakikisha unajenga msingi imara*
Ili kuweza kujenga msingi imara na utakaosaidia kuimarisha jengo lako zingatia mambo yafuatayo;
i.                 Fanya utafiti wa eneo lako hasa katika kutambua aina ya udongo
Hapa unaweza ukafanya hata utafiti wa macho tu na kwa kushirikiana na mtaalamu wako wa ujenzi ukaweza kufanya maamuzi ya msingi utakaohitajika. Wakati mwingine udongo wa juu ya ardhi unaweza ukawa tofauti na ule uliopo ndani ya ardhi baada ya kuchimba mita kadhaa na endapo utakutana na hali hii basi msingi wako itabidi ubadilike kulingana na aina ya udongo uliyokutana nayo. Cha kuzingatia hapa ni kuhakikisha msingi wako unakaa juu ya sehemu ngumu na imara ili kuepuka kutitia.

ii.               Tambua kama eneo lako lina maji maji au ni eneo kavu
Msingi unaojengwa sehemu zenye majimaji ni tofauti kabisa na msingi utakaojengwa sehemu kavu. Kwa eneo ambalo lina maji muda mrefu msingi wake utahitaji material (mali ghafi) zinazoweza kuhimili uwepo wa maji kama vile zege. Ukijenga msingi wa matofali ya kawaida kwenye eneo hili unajiweka kwenye hatari kubwa sana

iii.             Jua matumizi sahihi ya Jengo lako
Kwa kutambua matumizi sahihi ya jengo lako kunasaidia sana katika kutambua uzito sahihi utakaohitajika kubebwa na msingi wako. Msingi wa nyumba ya kuishi ni tofauti sana na msingi wa ghala hivyo usijenge nyumba ya kuishi hafu baada ya muda unaibadilisha na kuwa ghala utaleta matatizo kwenye msingi.

Ninachotaka kukukumbusha rafiki yangu leo ni kwamba msingi ndio sehemu ya kwanza muhimu kwenye jengo lako na kamwe hutakiwi kufanya makosa kwenye eneo hili.


Kitu kingine ambacho ningependa kusisitiza ni kwamba USIJENGE KWA MAZOEA. Epuka kabisa maneno ya mtaani eti mbona Fulani amejenga hivi au vile na wewe ukayapokea yalivyo. Itakapotokea tatizo itakuwa ni wewe na wale watakaokuwa wanaishi ndani ya nyumba hiyo.

Jenga msingi imara uwe na nyumba bora maisha yako yote.

Ni mimi rafiki yako na mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;
Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 (WhatsApp)
Blog: http://nyumbayakomaishayako.blogspot.com


Read More
      edit
Published March 10, 2019 by with 0 comment

Zifahamu Sababu Muhimu Za Kuweka Uzio Kwenye Eneo La Ujenzi



Habari ya leo rafiki yangu na mfatiliaji wa makala hizi bora kabisa za ujenzi. Ni matumaini yangu unaendelea kuchukua hatua muhimu ili kuhakikisha maisha yako na ya wale wanaokuzunguka yanakuwa bora kabisa!

Leo rafiki yangu karibu tujifunze kuhusu umuhimu wa kuweka uzio kwenye eneo la ujenzi. Inawezekana umewahi kupita sehemu yenye ujenzi ukakuta wamezungushia mabati kuzunguka eneo lote la ujenzi na ukawa unajiuliza kwanini wamefanya hivyo? Kuna sababu nzuri tu kwanini eneo la ujenzi huwa linazungushiwa uzio na hapa nakwenda kukueleza kwa kina sababu hizo. Lakini kabla hatujajifunza sababu za uzio huu hebu tuone kwanza, **Uzio wa eneo la Ujenzi (Site Hoarding), unamaanisha nini?**

Maana ya Uzio wa eneo la Ujenzi (Site Hoarding)
Huu ni aina ya uzio unaojengwa kwa matumizi ya muda mfupi (temporary structure) kuzunguka eneo la ujenzi. Ujenzi wa uzio huu ni muhimu sana na ni moja ya matakwa muhimu kutoka kwenye sheria za majenzi zinazotumika sehemu mbalimbali. Uzio huu unaweza kujengwa kwa mabati (Hii ndo mara nyingi inatumika), unaweza kujengwa pia kwa matofali au mabanzi kutegemeana na ukubwa/umuhimu wa project. Uzio huu pia hujengwa kabla ujenzi haujaanza na huondolewa pale ujenzi unapokamilika!

Mfano wa uzio wa mabati uliojengwa kuzunguka eneo la ujenzi.

Kwanini kuweka uzio eneo  la ujenzi??
Zifuatazo ni sababu muhimu za kuweka uzio kwenye eneo la ujenzi;

1.       Sababu ya kwanza na kubwa ni USALAMA (Health & Safety); uzio unahakikisha usalama wa wafanyakazi, wageni wanaokuja site pamoja na wanajamii wanaozunguka eneo la ujenzi. Eneo la ujenzi linaweza kuwa na mashimo, misumari, mizigo mizito… n,k hivyo usipoweka uzio ni rahisi kutokea ajali za hapa na pale na ajali nyingine zinaweza kuwa mbaya kabisa.

2.      Ulinzi na usalama wa mali zilizopo eneo la ujenzi. Kwenye eneo la ujenzi huwa kuna malighafi mbalimbali za kujengea na kama tunavyojua baadhi ya watu huwa sio waaminifu hivyo unapoweka uzio unapunguza uwezekano wa kuibiwa malighafi za ujenzi!

3.       Kuhakikisha watu sahihi tu ndio wanaingia eneo la ujenzi. Unapoweka uzio kunakuwa na geti maalumu la kuingilia na kutokea hivyo ni rahisi kuhakikisha wale wanaohusika na ujenzi tu ndio wanakuwa kwenye eneo la ujenzi.

4.       Kutumia sehemu hii ya uzio kuweka matangazo yanayohusiana na kampuni inayofanya ujenzi wa mradi husika. Kampuni inayofanya ujenzi inaweza kutumia uzio huu kujitangaza na kutafuta wateja zaidi kwa kuonyesha kile wanachofanya na uwezo wao kwa ujumla. Hii ni njia rahisi kabisa ya kujitangaza na kukuza biashara.

Mfano wa uzio wa nyavu za chuma kuzunguka eneo la ujenzi

Rafiki hayo ndio mambo muhimu zaidi linapokuja swala la uzio kwenye eneo la ujenzi. Zipo faida nyingine lakini kwa leo tuishie hapo. Cha msingi unapojenga uzio hakikisha uzio huo uko imara ili usiezuliwe na upepo kirahisi au kuharibiwa na watu kwa haraka. Uzio ni muhimu sana na unasaidia kutunza eneo lako la ujenzi.

Kwa ushauri kuhusu maswala yote yanayohusiana na ujenzi usisite kuwasiliana nami;
Rafiki yako mpendwa
Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084
Email : engbeatus.laswai@gmail.com

Read More
      edit
Published August 31, 2018 by with 0 comment

Je, unafahamu kwamba kuna vyoo maalumu kwa ajili ya Wazee/Walemavu na Watoto?




Habari ya leo rafiki yangu na mfatiliaji wa blogu hii nzuri kabisa ya “Nyumba Yako, Maisha Yako”. Nina Imani unaendelea kupambana vilivyo kuhakikisha unafanya dunia kuwa mahala salama na bora kabisa kuishi. Leo rafiki yangu karibu tujifunze kuhusu aina za vyoo ambavyo ni maalumu kwa ajili ya wazee, walemavu na watoto. Aina hizi za vyoo hazina utofauti sana na aina nyingine za kawaida bali zinakuwa zimefanyiwa maboresho kidogo ili kukidhi mahitaji ya makundi haya. Hivyo Kama unategemea kuishi na mzee au mlemavu au mtoto usijiumize kichwa sana, karibu tujifunze namna ya kuwasaidia kupata huduma bora kabisa ya choo.

Choo kwa Ajili Ya Wazee/Walemavu
                  
Kama tunavyojuwa rafiki swala la kujisogeza (movement) kwa wazee na walemavu ni swala gumu na linalohitaji usaidizi. Kwa kutambua changamoto hii, vyoo hivi vimefanyiwa maboresho makubwa mawili ili kuwasaidia watu hawa kujisaidia vizuri.

Boresho la kwanza ni kuweka sehemu ya kujishikiza ili kuwapa ufanisi wazee na walemavu wakati wanapotaka kukaa na wakati wa kuondoka baada ya kujisaidia. Sehemu hii ya kujishikiza inaweza ikatengenezwa ukutani karibu na choo kilipo au ikashikizwa kabisa kwenye choo.


Boresho la pili ni kuongeza urefu wa sehemu ya choo cha kukaa mpaka kufikia angalau 75cm. Choo cha kawaida kina urefu wa 50cm – 55cm. Urefu huu umeongezwa ili kuwapa urahisi wa kukaa bila kukunja miguu sana na hivyo kuwa na nguvu za kutosha wakati wa kuinuka baada ya kujisaidia.

Kwa kuzingatia maboresho haya mawili, mzee au mlemavu anaweza kujisaidia bila shida yoyote. Unapoanza ujenzi wa nyumba yako ni vyema ukakumbuka kuhusu hitaji hili la muhimu kabisa ili kuhakikisha unaandaa mazingira bora kwa ajili ya watu wa makundi yote.


Choo kwa Ajili Ya Watoto
      

Hivi ni vyoo maalumu hasa kwa watoto walio na umri kati ya miaka 3 hadi miaka 12. Vyoo hivi vinakuwa na umbo dogo kuliko vyoo vya kawaida ili kutoa urahisi kwa mtoto kujisaidia bila shida. Mfano vyoo vya kukaa urefu wake unakuwa kati ya 30cm mpaka 40cm.
Inashauriwa kutumia Zaidi vyoo vya kuchuchumaa kwa ajili ya watoto ili waweze kujisafisha vizuri na kujiepusha na hatari za magonjwa.


Choo cha watoto ni muhimu sana hasa kama unataka kuwajengea watoto utamaduni wa kujisaidia katika mazingira mazuri. Ubunifu huu unaweza ukafanyika sehemu mbalimbali kuanzia majumbani, hospitalini, kwenye mahoteli pamoja na sehemu nyingine.

Mpaka hapo rafiki yangu naamini kuna kitu kizuri umeweza kujifunza hasa kwa kutambua kwamba kuna namna bora kabisa ya kuhakikisha wazee, walemavu na watoto wanapata huduma bora ya choo. Hivyo utakapokuwa unafanya ujenzi ni vyema ukakumbuka elimu hii na kuifanyia kazi.
Ni mimi rafiki yako na mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;

Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 (WhatsApp)
Blog: nyumbayakomaishayako.blogspot.com



Read More
      edit