Published June 07, 2020 by with 0 comment

Zijue Faida Za Kutumia Wataalamu wa Ujenzi


Moja ya vitu ambavyo nimekuwa nikivitamani na kuhakikisha vinafanikiwa kwenye jamii yetu ni kusaidia kila mtu kuwa na nyumba bora ya kuishi. Katika maisha ya mwanadamu hapa duniani moja ya vitu muhimu sana ni kuwa na sehemu nzuri ya malazi. Jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi wamekuwa wakijenga kiholela bila kuwa na washauri na bila kufuata taratibu za kisheria. Ukiwauliza kwanini wanafanya hivyo watakwambia wanakwepa gharama lakini baada ya miaka kadhaa wanajikuta wapo kwenye majuto makubwa na mwisho wa siku wanaingia gharama mara mbili zaidi ya ambazo wangetumia mwanzoni kama wangefata utaratibu.

 

Baadhi ya watu niliokutana nao wamekuwa wakiniuliza Kuna umuhimu gani wa wao kutumia wataalamu wa ujenzi hasa wanapojenga nyumba za kawaida? Kwanini wasitumie tu mafundi wenye uzoefu?

Kama umekuwa ukifatilia makala zangu; moja ya makala nimeeleza vizuri kuhusu wataalamu wa ujenzi pamoja na vitu wanavyovifanya. Wataalamu hawa ni watu waliobobea katika sayansi ya mahesabu na ubunifu wa majengo. Kuna wahandisi (engineers), Wasanifu majengo (Architects) na Wakadiriaji majenzi (Quantity Surveyors).

SOMA HAPA: Wafahamu Wataalamu Wa Ujenzi

Leo hebu tuangalie ni kwanini unawahitaji watu hawa na usitumie tu mafundi pekee kwenye ujenzi wa nyumba yako. Zifuatazo ni sababu chache kati ya nyingi za kutumia wataalamu wa ujenzi;

i.          Ujenzi unatofautiana na kila nyumba ina mahitaji yake muhimu

Linapokuja swala la ujenzi kila mtu ana vionjo vyake anavyovitaka. Wataalamu wa ujenzi tofauti na mafundi ni watu waliosomea kwa kina namna bora ya kufanya nyumba ipendeze na kukidhi mahitaji yote muhimu kwa kuzingatia hitaji la mwenye nyumba. Ni rahisi zaidi kwa mtaalamu wa  ujenzi kujua mwenye nyumba anataka nini hasa kuliko ilivyo kwa fundi hivyo kwa kutumia mtaalamu wa ujenzi unajihakikishia kupata hasa kile unachohitaji.

 ii.        Mazingira ya ujenzi yanatofautiana

Njia ya ujenzi inayotumika kwenye eneo lenye majimaji ni tofauti kabisa na ujenzi wa eneo kavu. Eneo lenye maji pia linategemea kama maji hayo yanatembea au yamesimama na eneo kavu linaweza kuwa tambarare au lenye mwinuko. Fundi anaweza akawa mzuri eneo moja na kushindwa vibaya eneo jingine hivyo ili kuepuka hatari hii ni vizuri ukatafuta mtaalamu wa ujenzi atakayekuwa anampa ushauri na maelekezo fundi wako.

 iii.        Matumizi ya nyumba yanatofautiana

Nyumba iliyotengenezwa vizuri kwa kuzingatia matumizi sahihi ya jengo husika ni moja ya vitu muhimu sana katika kuhakikisha nyumba yako inadumu kwa muda mrefu bila kupoteza ubora wake. Mtaalamu wa ujenzi atashauri uimara unaohitajika kulingana na matumizi sahihi ya jengo husika kwa kuzingatia uzito (loading) na matumizi sahihi ya jengo lako.

 

Mbali na faida hizo hapo juu; faida nyingine za kutumia wataalamu hawa ni kama ifuatavyo;

  • Kupata ramani nzuri ya nyumba inayoendana na mahitaji yako pamoja na wakati wa sasa
  • Kupata makadirio ya vitu vinavyohitajika kwenye kila hatua ya ujenzi wa nyumba yako
  • Kupata mtu wa kumsimamia fundi na kuhakikisha anatengeneza kitu sahihi tena kwa ubora unaotakiwa
  • Kupata picha kamili ya ujenzi wa nyumba yako kabla hata hujaanza ujenzi.
  • Kupata ushauri sahihi pale unapotaka kubadili matumizi ya jengo lako au kama unataka kuongeza au kupunguza sehemu ya jengo

 

Faida ni nyingi, nyingi mnooo na kamwe hautakaa ujute eti kwa sababu ulitumia wataalamu wa ujenzi. Kizuri zaidi ni kwamba kwa sasa nchi yetu ina wataalamu wengi sana wa ujenzi wanaopatikana karibu yetu na kwa gharama nafuu kabisa. Usiogope chukua hatua sasa na tafuta mtaalamu atakayekushauri vyema kabla hujafanya makosa utakayokuja kuyajutia baadae.

Kwa ushauri kuhusu maswala ya ujenzi, usisite kuwasiliana nami

Rafiki yako mpendwa katika ujenzi wa taifa bora

Jina: Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com

 

Read More
      edit
Published May 31, 2020 by with 0 comment

Je unafahamu kuna Vyoo maalumu kwa Ajili ya Wazee/Walemavu na Watoto?



Habari ya leo rafiki yangu na mfatiliaji wa blogu hii nzuri kabisa ya “Nyumba Yako, Maisha Yako”. Nina Imani unaendelea kupambana vilivyo kuhakikisha unafanya dunia kuwa mahala salama na bora kabisa kuishi. Leo rafiki yangu karibu tujifunze kuhusu aina za vyoo ambavyo ni maalumu kwa ajili ya wazee, walemavu na watoto. Aina hizi za vyoo hazina utofauti sana na aina nyingine za kawaida bali zinakuwa zimefanyiwa maboresho kidogo ili kukidhi mahitaji ya makundi haya. Hivyo Kama unategemea kuishi na mzee au mlemavu au mtoto usijiumize kichwa sana, karibu tujifunze namna ya kuwasaidia kupata huduma bora kabisa ya choo.

 Choo kwa Ajili Ya Wazee/Walemavu

Kama tunavyojuwa rafiki swala la kujisogeza (movement) kwa wazee na walemavu ni swala gumu na linalohitaji usaidizi. Kwa kutambua changamoto hii, vyoo hivi vimefanyiwa maboresho makubwa mawili ili kuwasaidia watu hawa kujisaidia vizuri.

Boresho la kwanza ni kuweka sehemu ya kujishikiza ili kuwapa ufanisi wakati wanapotaka kukaa na wakati wa kuondoka baada ya kujisaidia. Sehemu hii ya kujishikiza inaweza ikatengenezwa ukutani karibu na choo kilipo au ikashikizwa kabisa kwenye choo.


Boresho la pili ni kuongeza urefu wa sehemu ya choo cha kukaa mpaka kufikia angalau 75cm. Choo cha kawaida kina urefu wa 50cm – 55cm. Urefu huu umeongezwa ili kuwapa urahisi wa kukaa bila kukunja miguu sana na hivyo kuwa na nguvu za kutosha wakati wa kuinuka baada ya kujisaidia.


Kwa kuzingatia maboresho haya mawili, mzee au mlemavu anaweza kujisaidia bila shida yoyote. Unapoanza ujenzi wa nyumba yako ni vyema ukakumbuka kuhusu hitaji hili la muhimu kabisa ili kuhakikisha unaandaa mazingira bora kwa ajili ya watu wa makundi yote.

Muhimu: Mtu yeyote anaweza kutumia choo cha wazee / walemavu lakini ni ngumu sana kwa mzee au mlemavu kutumia choo cha kawaida.

 Choo kwa Ajili Ya Watoto

Hivi ni vyoo maalumu hasa kwa watoto walio na umri chini ya miaka 12. Vyoo hivi vinakuwa na umbo dogo kuliko vyoo vya kawaida ili kutoa urahisi kwa mtoto kujisaidia bila shida. Mfano vyoo vya kukaa urefu wake unakuwa kati ya 30cm mpaka 40cm.

Nyumba nyingi za kisasa zimekuwa zikijengwa kwa kuhakikisha kila chumba kinakuwa na choo cha ndani kwa ndani (Self contained Rooms). Kwa kile chumba utakachoamua kwamba ni cha watoto basi ni vyema ukazingatia pia mahitaji ya choo yaendane na matumizi ya watoto.

Inashauriwa kutumia Zaidi vyoo vya kuchuchumaa kwa ajili ya watoto ili waweze kujisafisha vizuri na kujiepusha na hatari za magonjwa.

Choo cha watoto ni muhimu sana hasa kama unataka kuwajengea watoto utamaduni wa kujisaidia katika mazingira mazuri

 

Mpaka hapo rafiki yangu naamini kuna kitu kizuri umeweza kujifunza hasa kwa kutambua kwamba kuna namna bora kabisa ya kuhakikisha wazee, walemavu na watoto wanapata huduma bora ya choo. Hivyo utakapokuwa unafanya ujenzi ni vyema ukakumbuka elimu hii na kuifanyia kazi.

Ni mimi rafiki yako na mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;


Jina: Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
Read More
      edit
Published May 24, 2020 by with 0 comment

GHARAMA ZA UBUNIFU WA JENGO NA HASARA ZA KUEPUKA KUFANYA UBUNIFU WA JENGO






Moja ya jambo ambalo limekuwa likinishangaza kwenye ujenzi wa nyumba ni jinsi ambavyo watu wamekuwa wakipuuzia umuhimu wa ubunifu wa jengo kabla ya kuanza ujenzi. Wateja wengi wamekuwa wakiniambia ubunifu (design) ni kwa ajili ya ujenzi wa miradi mikubwa ya makampuni kitu ambacho si kweli hata kidogo. Jengo lolote (kuanzia majengo madogo ya kuishi mpaka majengo makubwa ya kibiashara) ni lazima kufanyiwa ubunifu wa kitaalamu ili kuhakikisha yanasimama imara na kuwa na muonekano unaotakiwa.
Nilichogundua ni kwamba watu wengi wana woga kuhusu gharama za ubunifu, baadhi ya wateja wanasema gharama ni kubwa sana, na wengine hawajui hata kama ujenzi unahitaji kuwa na mtaalamu wa ujenzi kwa ajili ya kufanya ubunifu.
Kuna mteta mmoja niliwahi kukutana naye alikuwa anataka kujenga nyumba ya ghorofa ambayo kwa haraka haraka gharama yake si chini ya Tshs mil 140 lakini alikuwa anataka ramani ya laki mbili. Tena akawa ananiambia kuna ramani huko mtaani eti zinauzwa kwa laki moja tu. Nilipomwambia aniletee hiyo ramani ya mtaani kwa bei hiyo na mimi nilipomwonyesha ramani ya nyumba nyingine iliyokamilika ndipo akagundua kuwa kinachouzwa mtaani ni sehemu ndogo sana sana ya kile kinachotakiwa na hakina manufaa yoyote kwenye ujenzi wa nyumba. Rafiki yangu ni muhimu kuwa makini sana maana siku hizi kumekuwa na matapeli wengi na taarifa nyingi za uwongo ambazo ni rahisi kukupoteza

Hasara za kuepuka kufanya ubunifu.
Umewahi kusikia jengo la ghorofa limedondoka? Umewahi kupita sehemu ukakuta nyumba ina mipasuko kama tetemeko limepita wakati nyumba nyingine ziko vizuri? N,k Kama umewahi kukutana na jengo ambalo limemalizika kujengwa halafu ndani ya muda mfupi likaanza kuonyesha udhaifu kama mipasuko au kubomoka basi kuna uwezekano mkubwa sana halikufanyiwa ubunifu yakinifu au wamenunua ramani sehemu na kuja kujenga bila kumhusisha mtaalamu wa ujenzi. Hasara kubwa ya kuepuka kufanya ubunifu wa ujenzi ni kupata jengo lisilokidhi viwango vya majenzi. Hasara nyingine kubwa ni kutumia gharama nyingi kuliko gharama halisi zinazohitajika kwa ujenzi wa jengo lako (Mbaya Zaidi ni kwamba utapoteza pesa nyingi na hutajua kama umepoteza pesa hizo).

Je ni gharama kiasi gani zinahitajika kwenye ubunifu?
Kabla sijakuambia gharama zinakuwaje rafiki yangu ngoja nikueleze kitu kimoja muhimu. Hakuna kazi ngumu kama kazi ya kufikiria hasa katika zama hizi ambazo kuna kelele nyingi sana. Na moja ya vitu vinavyohitaji ufikiri wa hali ya juu ni UBUNIFU.  Unapompa mtaalamu wa ujenzi kazi ya kufanya ubunifu unampa kazi ya kufikiri kwa kina namna ya kupangilia na kuhakikisha uimara wa jengo lako kwa namna unavyotaka wewe na baada ya hapo akutengenezee ramani ya nyumba hiyo ili uweze kuitumia kufanya ujenzi. Hili si jambo rahisi hata kidogo hasa ukizingatia kila mteja ana matakwa yake ya tofauti kuhusu aina ya nyumba anayotaka kuishi.
Kwa kuangalia maelezo hayo hapo juu utagundua kuwa hakuna gharama moja ambayo inayoweza kutumika kwa kila jengo, bali kila jengo litakuwa na gharama yake ya ubunifu kulingana na mahitaji ya mteja. Jambo la kuzingatia ni kwamba kadiri mahitaji ya nyumba yanavyokuwa mengi ndivyo gharama za ubunifu zinavyokuwa kubwa.

 
Kwa uzoefu wangu wa kufanya ubunifu na kujenga majengo ya aina mbalimbali; gharama za ubunifu huwa ni kati ya Tshs laki tano na TShs mil 5 za kitanzania kutegemeana na mahitaji ya mteja. Kuna wakati inaweza ikawa chini ya hapo au juu ya hapo, jambo la msingi ni kuhakikisha unamweleza kwa kina mtaalamu wa ujenzi kuhusu kile unachokitaka ili aweze kukukadiria gharama stahiki kwa jengo lako.

Hali ya Kufikirisha
Bado kuna watu utawasikia wakilalamika gharama hizo zipo juu. Hebu fikiria mtu unataka kujenga nyumba yenye thamani ya Zaidi ya mil 90 lakini mtaalamu wa ujenzi anakufanyia ubunifu kwa gharama labda ya Tshs mil 1.5; Hivi kweli utasema gharama ziko juu? Epuka sana vitu vya bei rahisi rafiki hasa linapokuja swala la ujenzi maana nyumba ni moja ya sehemu muhimu sana ya maisha yako hapa duniani.

Usijenge kwa mazoea, Jenga kitaalamu Ili nyumba yako iwe na thamani siku zote.
Ni mimi rafiki yako na mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;

Jina: Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
Read More
      edit