Habari ya leo rafiki yangu mpendwa na mfatiliaji wa blogu
hii nzuri kabisa inayokuelimisha kuhusu mbinu bora za ujenzi pamoja na ushauri
kuhusu mambo muhimu yanayohusiana na ujenzi. Hongera sana kwa siku hii nyingine
tulivu kabisa ambapo tunaenda kufanya yaliyo bora na kutegemea kupata matokeo
bora kabisa.
Leo rafiki tuelimishane kidogo kuhusu wataalamu wa ujenzi ni
kina nani na wanahusika na nini hasa kwenye ujenzi?
Wataalamu wa Ujenzi
Wataalamu wa ujenzi ni watu waliosomea na kubobea katika
maswala ya ujenzi wa nyumba kuanzia kwenye utengenezaji wa ramani nzuri,
makadirio ya ujenzi pamoja na usimamizi wa ujenzi wenyewe. Watu hawa wana
uelewa mkubwa sana kuhusu aina mbalimbali za ujenzi na namna bora ya kufanya
ujenzi wako kwa kufuata taratibu za eneo husika.
Tunaishi kwenye zama ambazo kila mtu anahitaji kuwa na
nyumba bora ya kisasa yenye vigezo vyote muhimu na iliyojengwa kwa gharama
nafuu. Unapotumia wataalamu hawa unajihakikishia kupata kile kilicho bora
kabisa kwa viwango vya kimataifa na kwa gharama nzuri kabisa. Wafuatao ni
wataalamu watatu kati ya wengi ambao inabidi uwafahau na ujue wanafanya nn;
1: Msanifu Majengo (Archtect)
Huyu ni mtaalamu ambaye kazi yake ni kubuni na kutengeneza
mpangilio wa jengo kutokana na mahitaji ya mteja. Anachora ramani ili kuweka
mawazo ya mteja katika picha na kuonesha uhalisia wa kile anachohitaji mteja.
Mtu huyu ni muhimu sana kwani ndiye anayetafsiri na kuhakikisha Kile
anachohitaji mteja kinawekwa katika picha nzuuri na kisha ramani kwa ajili ya
kupata kibali na kuendelea na ujenzi
2: Mhandisi (Engineer)
Mtaalamu huyu amebobea katika sayansi ya mahesabu na ubunifu
kuhusiana na shughuli za ujenzi. Mhandisi anakuwa na uwezo na maarifa ya
kuunda, kutunza na kutengeneza majengo. Kazi yake kubwa ni kuhakikisha uimara
wa jengo unazingatiwa. Maswala yote yanayohusiana na nondo, zege, ubora wa
tofali, aina ya cement, ukubwa wa nguzo pamoja na aina za makenchi kwa ajili ya
paa hufanyiwa ubunifu na mhandisi. Hayo ni machache sana kati ya vitu vingi
anavyofanya engineer. Anatumia picha na ramani zilizotengenezwa na msanifu
majengo katika kufanya kazi zake. Huyu pia anatengeneza ramani.
3: Mkadiriaji Majenzi (Quantity Surveyor)
Huyu ni mtaalamu aliyebobea katika mahesabu ya kukadiria
gharama za ujenzi. Kabla hujaanza ujenzi ni vizuri ukawa na picha halisi ya
gharama utakazotumia ili kukamilisha ujenzi wako. Gharama hizi zitaandaliwa
vizuri sana na mtaalamu huyu. Mtaalamu
huyu hutumia michoro ya Archtect na Engineer katika kufanya makadirio.
Mpaka hapo tunakuwa tumewafahamu wataalamu watatu muhimu
kabisa wanaohitajika kwenye shughuli yoyote ya ujenzi wa nyumba. Kuwapata
wataalamu hawa kuna gharama utatumia. Gharama hizo ni ndogo sana ukilinganisha
na hasara ambayo ungeipata kama utafanya ujenzi bila kumshirikisha mtaalamu.
Sio lazima utumie wataalamu wote waliotajwa hapo juu lakini hakikisha unampata
hata mmoja tu kwa ajili ya ushauri na msaada kuliko kufanya kila kitu peke
yako.
Hatua Ya Kuchukua
Kama una wazo la kujenga nyumba yako ya aina yoyote ile ni
vyema ukatafuta connection ya mtaalamu wa ujenzi ili awe mshauri wako mkuu
kabla na wakati wa ujenzi. Usifikirie saana kuhusu gharama, fikiria Zaidi
kuhusu thamani utakayoipata kwenye nyumba yako. Jitofautishe na watu wengine,
acha kabisa kufanya ujenzi kwa mazoea! Wataalamu wapo ili kuhakikisha unakuwa
na nyumba bora, ya kisasa, inayovutia na inayokidhi mahitaji yako ya sasa na ya
baadaye. Ni jukumu lako kuhakikisha unawatumia watu hawa vizuri
Nakutakia kila la kheri katika kuchukua hatua muhimu za
ujenzi na kufanya maisha yako kuwa bora kabisa.
#JengaKitaalamu
#TumiaWataalamuWaUjenzi
#EpukaKufanyaMakosaYasiyoYaLazima
#OkoaGharamaZaUjenzi
Kwa mahitaji kuhusu ushauri na namna bora ya kufanya ujenzi
wa nyumba yako usisite kuwasiliana nami
Jina : Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 (WhatsApp) or 0782 129 412 or 0712 877 343
Email : engbeatus.laswai@gmail.com
Blogy
: nyumbayakomaishayako.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment