Published March 03, 2020 by with 0 comment

UTARATIBU WA KUPATA KIBALI CHA UJENZI WA MAJENGO (BUILDING PERMIT)



Ujenzi wa majengo ni moja ya shughuli ambazo zinafanyika kwa kasi katika maeneo mengi ya nchi yetu! Kufanya ujenzi ni ndoto ya watu wengi na ni jambo zuri sana lakini watu wengi wamejikuta kwenye matatizo mbalimbali kutokana na kukiuka ama kutokujua taratibu  zinazohitajika kufwata kabla, wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi!

Ili kuepuka changamoto hizi leo nimeona nikuandalie mambo muhimu unayohitaji kuyafahamu unapohitaji kibali cha ujenzi wa majengo. Yafuatayo ni mambo matano ya msingi ya kuzingatia;

  • Uwe na hati/udhibitisho wa umiliki wa kiwanja.

Hapa ni vizuri eneo lako liwe kwenye ramani ya mipango miji yaani liwe limepimwa na umepewa hati miliki. Eneo linapokuwa kwenye ramani ya mipango miji linakuwa limeainishwa matumizi yake kama ni eneo la makazi, eneo la biashara, eneo la ibada, shule,,,, n.k  Jambo hili ni la muhimu kwani ndio linakupa msingi wa maamuzi ya aina ya jengo utakalojenga!

  • Ubunifu wa Kitaalamu wa Jengo

Kutegemeana na aina ya jengo hapa utahitaji kutafuta mtaalamu/wataalamu wa ujenzi (inaweza kuwa Msanifu Majengo (Architect) au Mhandisi (Engineer)), ambao watakusaidia kufanya ubunifu wa kitaalamu wa jengo lako kwa kuzingatia vigezo vyote vya eneo husika! Unahitaji kuwa na jengo la kisasa, lenye mvuto, usalama wa kutosha na gharama nafuu na hivi vyote unavipata kwenye ubunifu.

  • Kujaza Fomu Serikali ya Mtaa

Kuna fomu maalumu za kujaza kutoka serikali ya mtaa unakoishi kwa ajili ya kwenda kuombea kibali halmashauri/ manispaa husika

  • Kupeleka Michoro na Fomu ya Maombi Halmashauri/ Manispaa

Kutoka kwenye ubunifu utapewa michoro mbalimbali inayoonyesha muonekano wa jengo lako kuanzia kwenye msingi mpaka kwenye paa. Michoro hii utaambatanisha na fomu kutoka serikali ya mtaa na kupeleka manispaa. Michoro yote inabidi iwe imepigwa mihuri na sahihi ya mtaalamu wa ujenzi aliyesajiliwa. Hapa mtaalamu wako wa ujenzi anaweza kukusaidia kupeleka michoro na kukufanyia mchakato wa kuomba kibali. Kwa upande wa Architect huwa inapelekwa seti tatu za michoro na kwa upande wa Engineer huwa inapelekwa seti mbili za michoro pamoja na ripoti ya mahesabu ya ubunifu (Design Calculation Report).

  • Gharama na Muda wa Kutoa Kibali

Ukishakabidhi michoro manispaa husika kuna gharama kidogo ambazo utahitaji kulipia ili uweze kupata kibali. Gharama hizi zinatofautiana baina ya jengo na jengo kuanzia kwenye ukubwa wa jengo mpaka kwenye matumizi ya jengo husika. Ukifika manispaa michoro itakaguliwa na kisha utakadiriwa gharama za kibali ambazo utalipia na kisha utapewa risiti halafu hatua nyingine zitaendelea mpaka pale utakapopewa taarifa kwamba kibali chako kimetoka ambapo kwa siku hizi haichukui muda mrefu sana hasa kama jengo lako limefata vigezo vyote. Kwa mujibu wa kifungu cha 35 (i) cha sharia ya mipangomiji No. 8 ya mwaka 2007, Mamlaka ya upangaji inatakiwa kutoa kibali cha ujenzi katika kipindi kisichozidi SIKU 60 tangu mwombaji alipowasilisha maombi yake. Aidha ndani ya kipindi hicho mamlaka inatakiwa kumtaarifu mwombaji kama amekubaliwa au amekataliwa maombi yake na kutaja sababu zilizopelekea ombi lake kukataliwa.



Hizo ndio hatua muhimu rafiki ambazo unahitaji kuzijua unapohitaji kibali cha ujenzi wa jengo lako! Usisite kuwasiliana na mtaalamu wako wa ujenzi kwa usaidizi na maelekezo zaidi! 

KUMBUKA: Kufanya ujenzi hasa wa jengo lolote kiholela bila kibali kunaweza kukuweka kwenye matatizo makubwa ikiwemo kusimamishwa ujenzi na kupigwa faini ya fedha ambayo ni kubwa sana ukilinganisha na gharama ambazo ungetumia wakati wa usajili. Unaweza kuepuka haya yote kwa kuzingatia ushauri nilioelekeza hapo juu.

Asante sana kwa kuwa nami;
Jina: Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com

Read More
      edit