Published June 07, 2020 by with 0 comment

Zijue Faida Za Kutumia Wataalamu wa Ujenzi


Moja ya vitu ambavyo nimekuwa nikivitamani na kuhakikisha vinafanikiwa kwenye jamii yetu ni kusaidia kila mtu kuwa na nyumba bora ya kuishi. Katika maisha ya mwanadamu hapa duniani moja ya vitu muhimu sana ni kuwa na sehemu nzuri ya malazi. Jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi wamekuwa wakijenga kiholela bila kuwa na washauri na bila kufuata taratibu za kisheria. Ukiwauliza kwanini wanafanya hivyo watakwambia wanakwepa gharama lakini baada ya miaka kadhaa wanajikuta wapo kwenye majuto makubwa na mwisho wa siku wanaingia gharama mara mbili zaidi ya ambazo wangetumia mwanzoni kama wangefata utaratibu.

 

Baadhi ya watu niliokutana nao wamekuwa wakiniuliza Kuna umuhimu gani wa wao kutumia wataalamu wa ujenzi hasa wanapojenga nyumba za kawaida? Kwanini wasitumie tu mafundi wenye uzoefu?

Kama umekuwa ukifatilia makala zangu; moja ya makala nimeeleza vizuri kuhusu wataalamu wa ujenzi pamoja na vitu wanavyovifanya. Wataalamu hawa ni watu waliobobea katika sayansi ya mahesabu na ubunifu wa majengo. Kuna wahandisi (engineers), Wasanifu majengo (Architects) na Wakadiriaji majenzi (Quantity Surveyors).

SOMA HAPA: Wafahamu Wataalamu Wa Ujenzi

Leo hebu tuangalie ni kwanini unawahitaji watu hawa na usitumie tu mafundi pekee kwenye ujenzi wa nyumba yako. Zifuatazo ni sababu chache kati ya nyingi za kutumia wataalamu wa ujenzi;

i.          Ujenzi unatofautiana na kila nyumba ina mahitaji yake muhimu

Linapokuja swala la ujenzi kila mtu ana vionjo vyake anavyovitaka. Wataalamu wa ujenzi tofauti na mafundi ni watu waliosomea kwa kina namna bora ya kufanya nyumba ipendeze na kukidhi mahitaji yote muhimu kwa kuzingatia hitaji la mwenye nyumba. Ni rahisi zaidi kwa mtaalamu wa  ujenzi kujua mwenye nyumba anataka nini hasa kuliko ilivyo kwa fundi hivyo kwa kutumia mtaalamu wa ujenzi unajihakikishia kupata hasa kile unachohitaji.

 ii.        Mazingira ya ujenzi yanatofautiana

Njia ya ujenzi inayotumika kwenye eneo lenye majimaji ni tofauti kabisa na ujenzi wa eneo kavu. Eneo lenye maji pia linategemea kama maji hayo yanatembea au yamesimama na eneo kavu linaweza kuwa tambarare au lenye mwinuko. Fundi anaweza akawa mzuri eneo moja na kushindwa vibaya eneo jingine hivyo ili kuepuka hatari hii ni vizuri ukatafuta mtaalamu wa ujenzi atakayekuwa anampa ushauri na maelekezo fundi wako.

 iii.        Matumizi ya nyumba yanatofautiana

Nyumba iliyotengenezwa vizuri kwa kuzingatia matumizi sahihi ya jengo husika ni moja ya vitu muhimu sana katika kuhakikisha nyumba yako inadumu kwa muda mrefu bila kupoteza ubora wake. Mtaalamu wa ujenzi atashauri uimara unaohitajika kulingana na matumizi sahihi ya jengo husika kwa kuzingatia uzito (loading) na matumizi sahihi ya jengo lako.

 

Mbali na faida hizo hapo juu; faida nyingine za kutumia wataalamu hawa ni kama ifuatavyo;

  • Kupata ramani nzuri ya nyumba inayoendana na mahitaji yako pamoja na wakati wa sasa
  • Kupata makadirio ya vitu vinavyohitajika kwenye kila hatua ya ujenzi wa nyumba yako
  • Kupata mtu wa kumsimamia fundi na kuhakikisha anatengeneza kitu sahihi tena kwa ubora unaotakiwa
  • Kupata picha kamili ya ujenzi wa nyumba yako kabla hata hujaanza ujenzi.
  • Kupata ushauri sahihi pale unapotaka kubadili matumizi ya jengo lako au kama unataka kuongeza au kupunguza sehemu ya jengo

 

Faida ni nyingi, nyingi mnooo na kamwe hautakaa ujute eti kwa sababu ulitumia wataalamu wa ujenzi. Kizuri zaidi ni kwamba kwa sasa nchi yetu ina wataalamu wengi sana wa ujenzi wanaopatikana karibu yetu na kwa gharama nafuu kabisa. Usiogope chukua hatua sasa na tafuta mtaalamu atakayekushauri vyema kabla hujafanya makosa utakayokuja kuyajutia baadae.

Kwa ushauri kuhusu maswala ya ujenzi, usisite kuwasiliana nami

Rafiki yako mpendwa katika ujenzi wa taifa bora

Jina: Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 / 0782 129 412
Email : engbeatus.laswai@gmail.com

 

Read More
      edit