Leo rafiki yangu napenda kukushirikisha umuhimu wa kuwa na
msingi imara. Utaweza kufahamu msingi imara ni upi na ni kwa namna gani
utahakikisha unakuwa na msingi imara kabisa ili ujihakikishie ujenzi wa nyumba
bora.
*Msingi Imara* kwa ufupi ni ule ambao unaweza kuhimili uzito
wa jengo pamoja na nguvu kutoka nje kama vile upepo, msukumo wa udongo,
mitikisiko pamoja na nguvu nyingine za asili. Msingi huu unaweza ukajengwa kwa kutumia
mawe, matofali ya block, Zege au malighafi nyingine ambazo zinakubalika kwenye
ujenzi. Unapokuwa na msingi imara unajihakikishia usalama wako, mali zako na
wote watakaoishi ndani ya nyumba yako na pia utaweza kujikinga kwa namna Fulani
na majanga ya asili kama vile matetemeko na mitikisiko ya ardhi.
SOMA HAPA: Hatua Tatu Muhimu Ujenzi wa Msingi Imara
SOMA HAPA: Hatua Tatu Muhimu Ujenzi wa Msingi Imara
*Namna ya kuhakikisha unajenga msingi imara*
Ili kuweza kujenga msingi imara na utakaosaidia kuimarisha
jengo lako zingatia mambo yafuatayo;
i. Fanya utafiti wa eneo lako hasa katika kutambua
aina ya udongo
Hapa unaweza ukafanya hata utafiti wa macho tu na kwa kushirikiana na
mtaalamu wako wa ujenzi ukaweza kufanya maamuzi ya msingi utakaohitajika.
Wakati mwingine udongo wa juu ya ardhi unaweza ukawa tofauti na ule uliopo
ndani ya ardhi baada ya kuchimba mita kadhaa na endapo utakutana na hali hii
basi msingi wako itabidi ubadilike kulingana na aina ya udongo uliyokutana
nayo. Cha kuzingatia hapa ni kuhakikisha msingi wako unakaa juu ya sehemu ngumu
na imara ili kuepuka kutitia.
ii. Tambua kama eneo lako lina maji maji au ni eneo
kavu
Msingi unaojengwa sehemu zenye majimaji ni tofauti kabisa na msingi
utakaojengwa sehemu kavu. Kwa eneo ambalo lina maji muda mrefu msingi wake
utahitaji material (mali ghafi) zinazoweza kuhimili uwepo wa maji kama vile
zege. Ukijenga msingi wa matofali ya kawaida kwenye eneo hili unajiweka kwenye
hatari kubwa sana
iii. Jua matumizi sahihi ya Jengo lako
Kwa
kutambua matumizi sahihi ya jengo lako kunasaidia sana katika kutambua uzito
sahihi utakaohitajika kubebwa na msingi wako. Msingi wa nyumba ya kuishi ni
tofauti sana na msingi wa ghala hivyo usijenge nyumba ya kuishi hafu baada ya
muda unaibadilisha na kuwa ghala utaleta matatizo kwenye msingi.
Ninachotaka kukukumbusha rafiki yangu leo ni kwamba msingi ndio
sehemu ya kwanza muhimu kwenye jengo lako na kamwe hutakiwi kufanya makosa
kwenye eneo hili.
Kitu kingine ambacho ningependa kusisitiza ni kwamba
USIJENGE KWA MAZOEA. Epuka kabisa maneno ya mtaani eti mbona Fulani amejenga
hivi au vile na wewe ukayapokea yalivyo. Itakapotokea tatizo itakuwa ni wewe na
wale watakaokuwa wanaishi ndani ya nyumba hiyo.
Jenga msingi imara uwe na nyumba bora maisha yako yote.
SOMA PIA; UTARATIBU WA KUPATA KIBALI CHA UJENZI
Ni mimi rafiki yako na
mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;
Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084 (WhatsApp)
Email : engbeatus.laswai@gmail.com