Published March 10, 2019 by with 0 comment

Zifahamu Sababu Muhimu Za Kuweka Uzio Kwenye Eneo La Ujenzi



Habari ya leo rafiki yangu na mfatiliaji wa makala hizi bora kabisa za ujenzi. Ni matumaini yangu unaendelea kuchukua hatua muhimu ili kuhakikisha maisha yako na ya wale wanaokuzunguka yanakuwa bora kabisa!

Leo rafiki yangu karibu tujifunze kuhusu umuhimu wa kuweka uzio kwenye eneo la ujenzi. Inawezekana umewahi kupita sehemu yenye ujenzi ukakuta wamezungushia mabati kuzunguka eneo lote la ujenzi na ukawa unajiuliza kwanini wamefanya hivyo? Kuna sababu nzuri tu kwanini eneo la ujenzi huwa linazungushiwa uzio na hapa nakwenda kukueleza kwa kina sababu hizo. Lakini kabla hatujajifunza sababu za uzio huu hebu tuone kwanza, **Uzio wa eneo la Ujenzi (Site Hoarding), unamaanisha nini?**

Maana ya Uzio wa eneo la Ujenzi (Site Hoarding)
Huu ni aina ya uzio unaojengwa kwa matumizi ya muda mfupi (temporary structure) kuzunguka eneo la ujenzi. Ujenzi wa uzio huu ni muhimu sana na ni moja ya matakwa muhimu kutoka kwenye sheria za majenzi zinazotumika sehemu mbalimbali. Uzio huu unaweza kujengwa kwa mabati (Hii ndo mara nyingi inatumika), unaweza kujengwa pia kwa matofali au mabanzi kutegemeana na ukubwa/umuhimu wa project. Uzio huu pia hujengwa kabla ujenzi haujaanza na huondolewa pale ujenzi unapokamilika!

Mfano wa uzio wa mabati uliojengwa kuzunguka eneo la ujenzi.

Kwanini kuweka uzio eneo  la ujenzi??
Zifuatazo ni sababu muhimu za kuweka uzio kwenye eneo la ujenzi;

1.       Sababu ya kwanza na kubwa ni USALAMA (Health & Safety); uzio unahakikisha usalama wa wafanyakazi, wageni wanaokuja site pamoja na wanajamii wanaozunguka eneo la ujenzi. Eneo la ujenzi linaweza kuwa na mashimo, misumari, mizigo mizito… n,k hivyo usipoweka uzio ni rahisi kutokea ajali za hapa na pale na ajali nyingine zinaweza kuwa mbaya kabisa.

2.      Ulinzi na usalama wa mali zilizopo eneo la ujenzi. Kwenye eneo la ujenzi huwa kuna malighafi mbalimbali za kujengea na kama tunavyojua baadhi ya watu huwa sio waaminifu hivyo unapoweka uzio unapunguza uwezekano wa kuibiwa malighafi za ujenzi!

3.       Kuhakikisha watu sahihi tu ndio wanaingia eneo la ujenzi. Unapoweka uzio kunakuwa na geti maalumu la kuingilia na kutokea hivyo ni rahisi kuhakikisha wale wanaohusika na ujenzi tu ndio wanakuwa kwenye eneo la ujenzi.

4.       Kutumia sehemu hii ya uzio kuweka matangazo yanayohusiana na kampuni inayofanya ujenzi wa mradi husika. Kampuni inayofanya ujenzi inaweza kutumia uzio huu kujitangaza na kutafuta wateja zaidi kwa kuonyesha kile wanachofanya na uwezo wao kwa ujumla. Hii ni njia rahisi kabisa ya kujitangaza na kukuza biashara.

Mfano wa uzio wa nyavu za chuma kuzunguka eneo la ujenzi

Rafiki hayo ndio mambo muhimu zaidi linapokuja swala la uzio kwenye eneo la ujenzi. Zipo faida nyingine lakini kwa leo tuishie hapo. Cha msingi unapojenga uzio hakikisha uzio huo uko imara ili usiezuliwe na upepo kirahisi au kuharibiwa na watu kwa haraka. Uzio ni muhimu sana na unasaidia kutunza eneo lako la ujenzi.

Kwa ushauri kuhusu maswala yote yanayohusiana na ujenzi usisite kuwasiliana nami;
Rafiki yako mpendwa
Eng Beatus B. Laswai
Mobile : 0752 655 084
Email : engbeatus.laswai@gmail.com

Read More
      edit