Published November 18, 2019 by with 2 comments

Hatua Tatu Muhimu – Ujenzi wa Msingi Imara



Habari ya leo rafiki yangu na mfatiliaji wa blogu hii ya nyumba yako maisha yako. Leo ni siku nyingine ya kipekee kabisa ambapo tunaenda kufanya yaliyo bora na kutegemea kupata matokeo bora kabisa. Mimi kama mwalimu wako wa ujenzi naendelea kukuletea Makala bora kabisa ili ujifunze na kuhakikisha unafanikisha ndoto yako ya kuwa na nyumba bora kabisa.
Leo rafiki yangu tujifunze hatua tatu muhimu kwenye ujenzi wa msingi. Kama ambavyo tuliona kwenye moja ya Makala zilizopita, msingi ni sehemu muhimu kuliko zote kwenye ujenzi wa nyumba. Kama hukuisoma Makala hiyo isome hapa.

Ujenzi wa msingi unahitaji umakini wa kipekee ili kuhakikisha unakuwa na nyumba bora kabisa. Zifuatazo ni hatua tatu muhimu za kuzingatia katika ujenzi wa msingi;

Hatua Ya Kwanza: Isome na Kuielewa Vizuri Michoro ya Nyumba

Moja ya changamoto kubwa niliyokutana nayo kwa mafundi wengi ni kukosea vipimo vya michoro. Wengi wanafanya ujenzi kwa mazoea bila kutumia utaalamu na kwa kuwa wenye nyumba wengi hawana utaalamu wa mambo ya ujenzi inakuwa ni ngumu kugundua tatizo hili. Unapokosea kipimo cha msingi unabadili kabisa muonekano wa nyumba yako kwani msingi unaathiri sehemu ya juu ya nyumba. Kuna watu ukioanisha kilichopo kwenye ramani na kilichojengwa unakuta kuna tofauti kubwa sana.
Kabla hujaanza ujenzi isome michoro yako vizuri na hakikisha umeielewa. Ikiwezekana mtafute mtaalamu wa ujenzi ili aweze kumsimamia fundi na kuhakikisha anafanya kile kilichopo kwenye michoro. Mwombe akueleweshe na wewe ili ujue namna msingi wako utakavyokaa, nyumba yako ni ya thamani sana usikubali ijengwe kiholela.


Hatua Ya Pili: Chimba Msingi Mpaka Kwenye Kina Kinachokubalika

Msingi imara lazima ujengwe juu ya ardhi ngumu (mwamba). Sehemu ya juu ya ardhi huwa ni laini (dhaifu) na haifai kwa ajili ya kubeba msingi na nyumba yako kwa ujumla, hivyo ili kuwa na msingi imara huna budi kuchimba mpaka kwenye kina cha ardhi ngumu. Umbali kutoka juu ya ardhi mpaka ulipo mwamba unatofautiana baina ya sehemu na sehemu; usije ukaona rafiki yako kwenye eneo lake amechimba kidogo akaweka msingi na wewe ukaiga wakati eneo lako lipo sehemu tofauti.
Epuka kabisa mazoea kwenye ujenzi wa nyumba, kuna wakati eneo linaweza kuwa moja lakini lina sifa tofauti za udongo. Unaweza kuta pia eneo lako liliwahi kutumika kama sehemu ya kutupa takataka kipindi cha nyuma, unapojenga eneo hili utatumia mbinu tofauti kabisa na yule anayejenga eneo la kawaida. Unapochimba ni vizuri mtaalamu wa ujenzi akawepo ili aweze kukupa ushauri wa kitaalamu. Kuna wakati mwamba mgumu unaweza ukawa uko mbali sana na hivyo badala ya kuendelea kuchimba tunafanya maboresho kwenye udongo (soil improvement) ili kuupa udongo nguvu ya kubeba mzigo kutoka juu.


Hatua Ya Tatu: Tumia Malighafi Zenye Ubora

Moja ya changamoto kubwa kwenye ujenzi wa nyumba ni watu kupenda kutumia malighafi za bei nafuu ili kukwepa gharama. Hili limewafanya wengi kuingia kwenye gharama kubwa za matengenezo (au hata kubomoa sehemu iliyojengwa) kutokana na ujenzi kutokidhi viwango vya ubora.
Endapo unataka uwe na msingi imara na utakaodumu kwa muda mrefu ni lazima utumie malighafi zenye ubora wa hali ya juu. Kama msingi wako unajengwa kwa mawe basi tumia jiwe gumu kabisa, kama unajenga kwa matofali ya bloku basi tumia tofali zilizotengenezwa vizuri, kama unahitaji udongo kurudishia kwenye eneo la msingi hakikisha hautumii udongo wenye tope au mfinyanzi bali tumia mchanga wa mtoni au kifusi kilichokaguliwa na kukubalika.
Hata kama uwe na fundi mzuri kiasi gani, kama utatumia malighafi za kiwango cha chini basi tegemea kupata nyumba mbovu. Ni bora ujenge nyumba yako taratibu lakini kwa kiwango kinachokubalika kuliko kujenga haraka haraka halafu baada ya muda unaanza kuhangaika.

Mpaka hapo rafiki yangu naamini utakuwa umepata uelewa wa namna ya kuhakikisha unapata msingi imara wa nyumba yako utakaodumu miaka na miaka. Jambo la msingi ni kuhakikisha unapata mtaalamu wa ujenzi atakayekushauri namna bora ya kujenga msingi wa nyumba yako. Hata kama una fedha kidogo usiogope, sio kila ujenzi wa nyumba unahitaji gharama kubwa.

Ni mimi rafiki yako na mhamasishaji wa maswala ya ujenzi;
Eng Beatus B. Laswai
Mobile: 0752 655 084 (WhatsApp)
Email: engbeatus.laswai@gmail.com
Blog: http://nyumbayakomaishayako.blogspot.com

Read More
      edit